Open top menu
Alhamisi, 12 Desemba 2013
NEYMAR APIGA HAT TRICK YA KWANZA ULAYA BARCA IKIUA 6-1, ARSENAL YAPENYEA TUNDU LA SINDANO 16 BORA

KLABU ya Barcelona jana iliingia hatua ya 16 Bora kwa kishindo baada ya kuitandika Celtics mabao 6-1 huku mshambuliaji wake wa  Brazil, Neymar akipiga hat-trick yake ya kwanza barani Ulaya.

Licha ya Barcelona kuwakosa Andres Iniesta aliyebaki benchi, Leonel Messi ambaye bado majeruhi na Cesc Fabregas anayetumikia adhabu, imeendeleza makali yake ya kutoa kichapo hicho cha mbwa mwizi.

Neymar aliyeongoza safu ya ushambuliaji hakufanya makosa baada ya kufunga hat trick yake ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa dakika za 45, 48 na 58, wakati mabao mengine yalifungwa na Pique dakika ya saba, Pedro dakika ya 39, na Tello dakika ya 72. 

Kwa upande wa Arsenal wao wameponea chupuchupu kukosa hatua ya 16 bora baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Napoli ya Italia na kufanya timu zote tatu za kundi F zikifungana kwa pointi baada ya kumaliza wakiwa na pointi 12 na mabao ndiyo yaliyoipeleka hatua ya mtoano.

Arsenal ambayo walimaliza mchezo huyo wakiwa pungufu baada ya dakika ya 76, nahodha wake, Mikel Arteta alipotolewa nje kwa kadi nyekundu hali iliyosababisha kuleta udhaifu katika kikosi cha Arsene Wenger. 

Mabao ya Napoli yamefungwa na Gonzalo Higuain dakika ya 73 Callejon dakika ya 90.

Katika mchezo mwingine, timu ya Chelsea ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 bao pekee lilofungwa na Demba Ba dakika ya 11, limempa faraja kocha Jose Mourinho wa Chelsea kwa ushindi huo dhidi ya Steaua Bucharest.

Mapema mchana wa jana katika mchezo wa kiporo, bao pekee la Wesley Sneijder liliipa ushindi wa 1-0 nyumbani Galatasaray dhidi ya Juventus na kufuzu 16 Bora, huku Kibibi Kizee cha Turin kikifungishwa virago. 


Katika mechi nyingine za usiku huu, Marseille imefungwa 2-1 nyumbani na Borussia Dortmund, Atletico de Madrid imeidunga 2 - 0 FC Porto, FC Schalke 04 imeifunga 2 - 0 Basel, FK Austria Wien imeifunga 4-1 Zenit St Petersburg, AC Milan imetoka sare ya  0-0 na Ajax.

Read more
Jumanne, 10 Desemba 2013
  KILI STARS YASHINDWA KUHARIBU UHURU WA KENYA

TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imeshindwa kuvuruga sherehe za Uhuru wa Kenya ambapo kilele chake kinafanyika Desemba 12 ambayo ndiyo siku ya fainali ya Kombe la Challenge.

Kilimanjaro Stars kama ingeifunga Kenya katika hatua ya nusu fainali ya leo usiku, timu hiyo isingeweza kucheza fainali na kutwaa kombe katika sherehe za kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Kenya.

Kili Stars imekubali kipigo cha bao 1-0 na Kenya ‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, usiku huu ikisindikizwa na mvua.

Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu keshokutwa mchana Uwanja wa Nyayo tena, wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.

Mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbwana Samatta akiwatoka mabeki wa Kenya, Joackins Atudo kulia na Aboud Omar kushoto Nyayo usiku huu.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Thiery Nkurunziza wa Burundi, aliyesaidiwa na Idam Hamid wa Sudan na Mussie Kinde wa Ethiopia, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na kumchungulia kipa Ivo Mapunda.
Baada ya bao hilo, Stars walizinduka na kuanza kushambulia, lakini ukuta wa Kenya ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote.

Nafasi pekee nzuri ambayo Stars waliipata ilikuwa dakika ya 44, wakati kona nzuri ya Mrisho Ngassa ilipopanguliwa na kipa Duncan Ochieng, lakini Mbwana Samatta akachelewa kuunganisha, Joackins Atudo akaondosha kwenye hatari.

Kipindi cha Stars ilicheza vizuri zaidi, lakini bado ukuta wa Harambee ulikuwa mgumu na nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho ilikuwa dakika ya 88, wakati Mbwana Samatta alipomtoka beki wa Kenya na kuingia vizuri ndani ya 18, lakini akapiga juu.


Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa wakilia na ikabidi viongozi wachukue jukumu la kuwabembeleza. Nahidha Kevin Yondan ndiye alikuwa ana hali mbaya zaidi. 
Read more
FAINALI BALLON D'OR NI MESSI, RONALDO AU RIBBERY

FIFA imethibitisha orodha ya majina ya wachezaji watatu walioingia fainali ya kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa mwaka 2013, Ballon d'Or ambao ni mtetezi Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Franck Ribery.

Messi ameshinda mfululizo mara nne tuzo zilizopita, lakini safari hii ni Ronaldo anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa mpira wa dhahabu.

Mshindi mtarajiwa, Messi anaweza kupokonywa tuzo hiyo na Ronaldo kutokana na mchezaji huyo Real Madrid kuwa juu hivi sasa

Mshambuliaji huyo wa Real Madrid, amefunga mabao 32 tayari msimu huu kwa klabu na timu yake ya taifa, huku Messi kwa sasa yupo nje ya kikosi cha Barcelona kutokana na maumivu ya nyama.

Mabao yake matatu aliyofunga peke yake, hat-trick wakati Ureno inaifunga 3-2 Sweden katika mechi maalum ya kufuzu Kombe la Dunia, yameongeza hamasa za watu kumpendekeza kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili katika historia yake.

Ribery, aliyeiwezesha Bayern Munich kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuishinda kabla ya Ronaldo kufanya mambo makubwa dhidi ya Sweden na FIFA ikaongeza muda wa kupigia kura washindani.

Mshindi atatangazwa katika usiku wa hafla maalum ya Ballon d'Or mjini Zurich, Uswis Januari 13, mwakani.

Wakati huo huo, FIFA pia imethibitisha orodha ya wachezaji wanaowania kuwamo katika kikosi cha wachezaji 11 bora wa dunia, FIFPro World XI 2013.

Kuna wachezaji wanne wa England kwenye orodha hiyo ambao ni Leighton Baines, Ashley Cole, Steven Gerrard na Wayne Rooney.

Wachezaji ambao wanatarajiwa kushindania kuingia katika kikosi hicho ni:-
Makipa:
Gianluigi Buffon (Italy, Juventus); Iker Casillas (Spain, Real Madrid CF); Petr Cech (Czech Republic, Chelsea FC); Manuel Neuer (Germany, FC Bayern München), Víctor Valdes (Spain, FC Barcelona).

Mabeki:
David Alaba (Austria, FC Bayern München); Jordi Alba (Spain, FC Barcelona); Dani Alves (Brazil, FC Barcelona); Leighton Baines (England, Everton FC); Jérôme Boateng (Germany, FC Bayern München);Ashley Cole (England, Chelsea FC); Dante (Brazil, FC Bayern München); Mats Hummels (Germany, Borussia Dortmund); Branislav Ivanović (Serbia, Chelsea FC); Vincent Kompany (Belgium, Manchester City FC); Philipp Lahm (Germany, FC Bayern München); David Luiz (Brazil, Chelsea FC); Marcelo (Brazil, Real Madrid CF); Pepe (Portugal, Real Madrid CF); Gerard Piqué (Spain, FC Barcelona); Sergio Ramos(Spain, Real Madrid CF ); Thiago Silva (Brazil, Paris St-Germain FC); Raphaël Varane (France, Real Madrid CF); Nemanja Vidić (Serbia, Manchester United FC); Pablo Zabaleta (Argentina, Manchester City FC).

Viungo:
Xabi Alonso (Spain, Real Madrid CF); Gareth Bale (Wales, Tottenham Hotspur FC/Real Madrid CF);Sergio Busquets (Spain, FC Barcelona); Steven Gerrard (England, Liverpool FC); Andrés Iniesta (Spain, FC Barcelona); Isco (Spain, Málaga CF/ Real Madrid CF); Mesut Özil (Germany, Real Madrid CF/Arsenal FC); Andrea Pirlo (Italy, Juventus); Marco Reus (Germany, Borussia Dortmund); Franck Ribéry (France, FC Bayern München), Arjen Robben (Netherlands, FC Bayern München); Bastian Schweinsteiger(Germany, FC Bayern München); Yaya Touré (Côte d’Ivoire, Manchester City FC); Arturo Vidal (Chile, Juventus); Xavi  (Spain; FC Barcelona).

Washambuliaji:

Sergio Agüero (Argentina, Manchester City FC); Mario Balotelli (Italy, Manchester City FC/AC Milan); Edinson Cavani (Uruguay, SSC Napoli/Paris Saint-Germain FC); Diego Costa (Spain, Club Atlético de Madrid); Cristiano Ronaldo (Portugal, Real Madrid CF); Didier Drogba (Côte d’Ivoire, Shanghai Shenhua FC/Galatasaray SK); Radamel Falcao (Colombia, Club Atlético de Madrid/AS Monaco FC); Zlatan Ibrahimovi (Sweden, Paris Saint-Germain FC); Robert Lewandowski (Poland, Borussia Dortmund); Mario Mandžukić (Croatia, FC Bayern München); Lionel Messi (Argentina, FC Barcelona); Neymar (Brazil, Santos FC/FC Barcelona); Wayne Rooney (England, Manchester United FC); Luis Suárez (Uruguay, Liverpool FC); Robin van Persie (Netherlands, Manchester United FC).
Read more
ALAN KAMOTE AMPIGA DEO SAMWELI KWA POINTI

Bondia Alan Kamote kulia akimshambulia Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es Salaam, Kamote alishinda kwa pointi. 


Bondia Alan Kamote kulia akipambana na Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es Salaam, Kamote alishinda kwa pointi.
Read more
Jumatatu, 9 Desemba 2013
MBURUNDI STAA MPYA WA TUSKER PROJECT FAME

MSHIRIKI aitwaye Hope toka Burundi amejikuta akianguka chini kwa mshituko wa furaha ulimkuta baada ya kuibuka kidedea kwa kutangazwa mshindi wa Tusker Project Fame na kujinyakulia kitita cha Shilingi 5,000,000/= za Kenya.

Mashindano hayo yaliyomalizika hivi punde usiku huu yamemwacha Hope katika taharuki huku akiwabwaga washiriki wenzake, Hisia (Tanzania), Patrick (Rwanda), Wambura (Kenya), Daisy (Uganda), Amos & Josh wa Kenya


Sauti ya pekee ya kijana huyo imeibua thamani yake katika tasnia ya muziki, Hope hakuwahi kufanya video ya wimbo wowote zaidi ya ule uliompatia ushindi wa Tusker.
Read more
ARSENAL YAVUTWA JEZI ENGLAND, BADO WAPO KILELENI

KLABU ya Arsenal jana ilipunguzwa kasi yake katika Ligi Kuu ya England baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Everton katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Emirates jijini London.

Arsenal ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo Mesut Ozil dakika ya 80, lakini Gerard Deulofeu aliyetokea benchi akaisawazishia Everton dakika ya 84 na kufanya timu hizo kugawana pointi katika mchezo huo. 

Everton hata hivyo hawakuwa na wasiwasi wa mchezaji yeyote kuwa na jeraha. Antolin Alcaraz alikuwa kwenye kikosi hicho lakini Leighton Baines, Arouna Kone na Darron Gibson walisalia nje.


Licha ya kuongoza orodha kwa pointi tano sasa, baadhi wana shauku ikiwa kweli Arsenal inaweza kushinda kombe hilo msimu huu kwa sababu ushawishi wao kuweza kufanya hivyo bado haujawagusa mashabiki wengi wa soka.

Read more
WATATU MBARONI KWA KUPANGA MATOKEO ENGLAND

WATU watatu wanashikiliwa na polisi nchini England baada ya aliyekuwa mchezaji wa Portsmouth kumwambia mwandishi wa habari kuwa alihusika katika kupanga mechi.

Sam Sodje alirekodiwa kwenye kanda ya video na mwandishi wa habari mmoja wa jarida la Sun akizungumzia alivyompiga mchezaji wa timu hasimu usoni katika ligi ya daraja la kwanza, ili apate kadi nyekundu na kisha baadaye alipwe pauni 70,000.

Alisema pia alipangia mchezaji mwingine aweze kulipwa pauni 30,000 kwa kupokea kadi ya njano katika mechi ya ligi. Klabu ya Portsmouth imeelezea kushtushwa sana na madai hayo.

Katika video hiyo liyorekodiwa kisiri, Sodje raia wa Nigeria, pia alidai ana uwezo wa kupanga mechi za ligi kuu na kuwa yuko tayari kupanga mechi katika kombe la dunia mwaka ujao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa klabu hiyo, alisema kuwa ikiwa madai haya ni ya kweli, basi ijulikane kuwa ni ya kushtua na kushangaza sana, jambo la kupanga mechi bila shaka linaathiri pakubwa maadili ya mchezo wa soka.


Sodje hachezei tena klabu ya Portsmouth lakini itambidi ashirikiane na maafisa wakuu kwa uchunguzi. Sodje aliondolewa uwanjani katika dakika ya 50 wakati wa mchuano kati ya Portsmouth na Oldham Athletic kwenye ligi ya daraja la kwanza 23 Februari mwaka 2013.
Read more
Jumapili, 8 Desemba 2013
KENYA WAWAPELEKA KILIMANJARO STARS MACHINJIONI KWENYE MATOPE

MECHI ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa Machakos.

Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa 64 kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10 mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja  na kituo cha televisheni cha SuperSport kupitia chaneli ya SS9.

Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Aga Khan katika Jiji la Mombasa.

Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars yalifungwa na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania nyavu ni Amri Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.


Read more
KIKWETE AMPONGEZA TENGA, AMBEBESHA ZIGO MALINZI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.

Ametoa changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.

Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.

Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.
Read more
PAMBANO LA TANZANITE LAINGIZA MIL 5/-

PAMBANO kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,732,012.01.

Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh. 6,190,000.


Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Read more
MAVETERANI MORO KUVAANA MWISHONI MWA WIKI HII

BONANZA la mchezo wa mpira wa miguu litakaloshirikisha timu mbalimbali za Veterani za mkoani Morogoro linatarajiwa kufanyika Desemba 14 na 15, mwaka huu, katika uwanja wa Shujaa, mjini hapa.

Akizungumza na mtandao huu, mratibu wa bonanza hilo, Daudi Julian alisema lengo la bonanza hilo, ni kuwakutanisha pamoja wanasoka wa zamani na kuimarisha afya zao.

Julian alisema maandalizi kuendelea bonanza hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa yanakwenda vizuri huku timu shiriki zikiwa katika mazoezi makali.

Mratibu huyo alizitaja baadhi ya timu zinazotarajia kushiriki katika bonanza hilo kuwa ni Moro Veterani, Reli Family Veterani, Kihonda Veterani, Mzumbe Veterani, Kichangani Veterani, Burkina Faso Veterani, Mazimbu Veterani na Shooting Stars Veterani.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na tayari baadhi ya timu zimethibitisha kushiriki,” alisema.

Aidha, Julian alisema zawadi mbalimbali zinatarajiwa kutolewa kwa timu zitakazofanya vizuri ikiwemo pia zawadi kwa mchezaji mmoja mmoja.


“Hili bonanza ni la aina yake na kwamba halijawahi kufanyika mkoani Morogoro na niseme huu ni mwanzo tu, mabonanza zaidi yanakuja,” alisema.
Read more