MICHUANO ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji
wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu inaanza kutimua vumbi Novemba
17 mwaka huu katika viwanja vya Karume na Azam Complex, Dar es Salaam.
Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Maji Uhai
imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari katika ofisi
za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo timu zimepangwa katika
makundi matatu.
Kundi A linaundwa na timu za Azam, Coastal Union,
JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti United, Mgambo
Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino
Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.
Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17 mwaka huu ni
kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume), Yanga na Mbeya City (saa
8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi-
Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Karume).
Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2 asubuhi- Azam)
na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam) ndizo zitakazocheza
mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi C.
Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa Novemba 24
na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27 mwaka huu. Mechi
ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali zitachezwa Novemba 30 mwaka.
0 comments