Open top menu
Alhamisi, 12 Desemba 2013
NEYMAR APIGA HAT TRICK YA KWANZA ULAYA BARCA IKIUA 6-1, ARSENAL YAPENYEA TUNDU LA SINDANO 16 BORA

KLABU ya Barcelona jana iliingia hatua ya 16 Bora kwa kishindo baada ya kuitandika Celtics mabao 6-1 huku mshambuliaji wake wa  Brazil, Neymar akipiga hat-trick yake ya kwanza barani Ulaya.

Licha ya Barcelona kuwakosa Andres Iniesta aliyebaki benchi, Leonel Messi ambaye bado majeruhi na Cesc Fabregas anayetumikia adhabu, imeendeleza makali yake ya kutoa kichapo hicho cha mbwa mwizi.

Neymar aliyeongoza safu ya ushambuliaji hakufanya makosa baada ya kufunga hat trick yake ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa dakika za 45, 48 na 58, wakati mabao mengine yalifungwa na Pique dakika ya saba, Pedro dakika ya 39, na Tello dakika ya 72. 

Kwa upande wa Arsenal wao wameponea chupuchupu kukosa hatua ya 16 bora baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Napoli ya Italia na kufanya timu zote tatu za kundi F zikifungana kwa pointi baada ya kumaliza wakiwa na pointi 12 na mabao ndiyo yaliyoipeleka hatua ya mtoano.

Arsenal ambayo walimaliza mchezo huyo wakiwa pungufu baada ya dakika ya 76, nahodha wake, Mikel Arteta alipotolewa nje kwa kadi nyekundu hali iliyosababisha kuleta udhaifu katika kikosi cha Arsene Wenger. 

Mabao ya Napoli yamefungwa na Gonzalo Higuain dakika ya 73 Callejon dakika ya 90.

Katika mchezo mwingine, timu ya Chelsea ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 bao pekee lilofungwa na Demba Ba dakika ya 11, limempa faraja kocha Jose Mourinho wa Chelsea kwa ushindi huo dhidi ya Steaua Bucharest.

Mapema mchana wa jana katika mchezo wa kiporo, bao pekee la Wesley Sneijder liliipa ushindi wa 1-0 nyumbani Galatasaray dhidi ya Juventus na kufuzu 16 Bora, huku Kibibi Kizee cha Turin kikifungishwa virago. 


Katika mechi nyingine za usiku huu, Marseille imefungwa 2-1 nyumbani na Borussia Dortmund, Atletico de Madrid imeidunga 2 - 0 FC Porto, FC Schalke 04 imeifunga 2 - 0 Basel, FK Austria Wien imeifunga 4-1 Zenit St Petersburg, AC Milan imetoka sare ya  0-0 na Ajax.

Read more
Jumanne, 10 Desemba 2013
  KILI STARS YASHINDWA KUHARIBU UHURU WA KENYA

TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imeshindwa kuvuruga sherehe za Uhuru wa Kenya ambapo kilele chake kinafanyika Desemba 12 ambayo ndiyo siku ya fainali ya Kombe la Challenge.

Kilimanjaro Stars kama ingeifunga Kenya katika hatua ya nusu fainali ya leo usiku, timu hiyo isingeweza kucheza fainali na kutwaa kombe katika sherehe za kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Kenya.

Kili Stars imekubali kipigo cha bao 1-0 na Kenya ‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, usiku huu ikisindikizwa na mvua.

Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu keshokutwa mchana Uwanja wa Nyayo tena, wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.

Mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbwana Samatta akiwatoka mabeki wa Kenya, Joackins Atudo kulia na Aboud Omar kushoto Nyayo usiku huu.

Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Thiery Nkurunziza wa Burundi, aliyesaidiwa na Idam Hamid wa Sudan na Mussie Kinde wa Ethiopia, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na kumchungulia kipa Ivo Mapunda.
Baada ya bao hilo, Stars walizinduka na kuanza kushambulia, lakini ukuta wa Kenya ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote.

Nafasi pekee nzuri ambayo Stars waliipata ilikuwa dakika ya 44, wakati kona nzuri ya Mrisho Ngassa ilipopanguliwa na kipa Duncan Ochieng, lakini Mbwana Samatta akachelewa kuunganisha, Joackins Atudo akaondosha kwenye hatari.

Kipindi cha Stars ilicheza vizuri zaidi, lakini bado ukuta wa Harambee ulikuwa mgumu na nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho ilikuwa dakika ya 88, wakati Mbwana Samatta alipomtoka beki wa Kenya na kuingia vizuri ndani ya 18, lakini akapiga juu.


Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa wakilia na ikabidi viongozi wachukue jukumu la kuwabembeleza. Nahidha Kevin Yondan ndiye alikuwa ana hali mbaya zaidi. 
Read more
FAINALI BALLON D'OR NI MESSI, RONALDO AU RIBBERY

FIFA imethibitisha orodha ya majina ya wachezaji watatu walioingia fainali ya kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa mwaka 2013, Ballon d'Or ambao ni mtetezi Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Franck Ribery.

Messi ameshinda mfululizo mara nne tuzo zilizopita, lakini safari hii ni Ronaldo anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa mpira wa dhahabu.

Mshindi mtarajiwa, Messi anaweza kupokonywa tuzo hiyo na Ronaldo kutokana na mchezaji huyo Real Madrid kuwa juu hivi sasa

Mshambuliaji huyo wa Real Madrid, amefunga mabao 32 tayari msimu huu kwa klabu na timu yake ya taifa, huku Messi kwa sasa yupo nje ya kikosi cha Barcelona kutokana na maumivu ya nyama.

Mabao yake matatu aliyofunga peke yake, hat-trick wakati Ureno inaifunga 3-2 Sweden katika mechi maalum ya kufuzu Kombe la Dunia, yameongeza hamasa za watu kumpendekeza kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili katika historia yake.

Ribery, aliyeiwezesha Bayern Munich kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuishinda kabla ya Ronaldo kufanya mambo makubwa dhidi ya Sweden na FIFA ikaongeza muda wa kupigia kura washindani.

Mshindi atatangazwa katika usiku wa hafla maalum ya Ballon d'Or mjini Zurich, Uswis Januari 13, mwakani.

Wakati huo huo, FIFA pia imethibitisha orodha ya wachezaji wanaowania kuwamo katika kikosi cha wachezaji 11 bora wa dunia, FIFPro World XI 2013.

Kuna wachezaji wanne wa England kwenye orodha hiyo ambao ni Leighton Baines, Ashley Cole, Steven Gerrard na Wayne Rooney.

Wachezaji ambao wanatarajiwa kushindania kuingia katika kikosi hicho ni:-
Makipa:
Gianluigi Buffon (Italy, Juventus); Iker Casillas (Spain, Real Madrid CF); Petr Cech (Czech Republic, Chelsea FC); Manuel Neuer (Germany, FC Bayern München), Víctor Valdes (Spain, FC Barcelona).

Mabeki:
David Alaba (Austria, FC Bayern München); Jordi Alba (Spain, FC Barcelona); Dani Alves (Brazil, FC Barcelona); Leighton Baines (England, Everton FC); Jérôme Boateng (Germany, FC Bayern München);Ashley Cole (England, Chelsea FC); Dante (Brazil, FC Bayern München); Mats Hummels (Germany, Borussia Dortmund); Branislav Ivanović (Serbia, Chelsea FC); Vincent Kompany (Belgium, Manchester City FC); Philipp Lahm (Germany, FC Bayern München); David Luiz (Brazil, Chelsea FC); Marcelo (Brazil, Real Madrid CF); Pepe (Portugal, Real Madrid CF); Gerard Piqué (Spain, FC Barcelona); Sergio Ramos(Spain, Real Madrid CF ); Thiago Silva (Brazil, Paris St-Germain FC); Raphaël Varane (France, Real Madrid CF); Nemanja Vidić (Serbia, Manchester United FC); Pablo Zabaleta (Argentina, Manchester City FC).

Viungo:
Xabi Alonso (Spain, Real Madrid CF); Gareth Bale (Wales, Tottenham Hotspur FC/Real Madrid CF);Sergio Busquets (Spain, FC Barcelona); Steven Gerrard (England, Liverpool FC); Andrés Iniesta (Spain, FC Barcelona); Isco (Spain, Málaga CF/ Real Madrid CF); Mesut Özil (Germany, Real Madrid CF/Arsenal FC); Andrea Pirlo (Italy, Juventus); Marco Reus (Germany, Borussia Dortmund); Franck Ribéry (France, FC Bayern München), Arjen Robben (Netherlands, FC Bayern München); Bastian Schweinsteiger(Germany, FC Bayern München); Yaya Touré (Côte d’Ivoire, Manchester City FC); Arturo Vidal (Chile, Juventus); Xavi  (Spain; FC Barcelona).

Washambuliaji:

Sergio Agüero (Argentina, Manchester City FC); Mario Balotelli (Italy, Manchester City FC/AC Milan); Edinson Cavani (Uruguay, SSC Napoli/Paris Saint-Germain FC); Diego Costa (Spain, Club Atlético de Madrid); Cristiano Ronaldo (Portugal, Real Madrid CF); Didier Drogba (Côte d’Ivoire, Shanghai Shenhua FC/Galatasaray SK); Radamel Falcao (Colombia, Club Atlético de Madrid/AS Monaco FC); Zlatan Ibrahimovi (Sweden, Paris Saint-Germain FC); Robert Lewandowski (Poland, Borussia Dortmund); Mario Mandžukić (Croatia, FC Bayern München); Lionel Messi (Argentina, FC Barcelona); Neymar (Brazil, Santos FC/FC Barcelona); Wayne Rooney (England, Manchester United FC); Luis Suárez (Uruguay, Liverpool FC); Robin van Persie (Netherlands, Manchester United FC).
Read more
ALAN KAMOTE AMPIGA DEO SAMWELI KWA POINTI

Bondia Alan Kamote kulia akimshambulia Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es Salaam, Kamote alishinda kwa pointi. 


Bondia Alan Kamote kulia akipambana na Deo Samweli wakati wa mpambano wao uliofanyika Manzese Dar es Salaam, Kamote alishinda kwa pointi.
Read more
Jumatatu, 9 Desemba 2013
MBURUNDI STAA MPYA WA TUSKER PROJECT FAME

MSHIRIKI aitwaye Hope toka Burundi amejikuta akianguka chini kwa mshituko wa furaha ulimkuta baada ya kuibuka kidedea kwa kutangazwa mshindi wa Tusker Project Fame na kujinyakulia kitita cha Shilingi 5,000,000/= za Kenya.

Mashindano hayo yaliyomalizika hivi punde usiku huu yamemwacha Hope katika taharuki huku akiwabwaga washiriki wenzake, Hisia (Tanzania), Patrick (Rwanda), Wambura (Kenya), Daisy (Uganda), Amos & Josh wa Kenya


Sauti ya pekee ya kijana huyo imeibua thamani yake katika tasnia ya muziki, Hope hakuwahi kufanya video ya wimbo wowote zaidi ya ule uliompatia ushindi wa Tusker.
Read more
ARSENAL YAVUTWA JEZI ENGLAND, BADO WAPO KILELENI

KLABU ya Arsenal jana ilipunguzwa kasi yake katika Ligi Kuu ya England baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Everton katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Emirates jijini London.

Arsenal ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo Mesut Ozil dakika ya 80, lakini Gerard Deulofeu aliyetokea benchi akaisawazishia Everton dakika ya 84 na kufanya timu hizo kugawana pointi katika mchezo huo. 

Everton hata hivyo hawakuwa na wasiwasi wa mchezaji yeyote kuwa na jeraha. Antolin Alcaraz alikuwa kwenye kikosi hicho lakini Leighton Baines, Arouna Kone na Darron Gibson walisalia nje.


Licha ya kuongoza orodha kwa pointi tano sasa, baadhi wana shauku ikiwa kweli Arsenal inaweza kushinda kombe hilo msimu huu kwa sababu ushawishi wao kuweza kufanya hivyo bado haujawagusa mashabiki wengi wa soka.

Read more
WATATU MBARONI KWA KUPANGA MATOKEO ENGLAND

WATU watatu wanashikiliwa na polisi nchini England baada ya aliyekuwa mchezaji wa Portsmouth kumwambia mwandishi wa habari kuwa alihusika katika kupanga mechi.

Sam Sodje alirekodiwa kwenye kanda ya video na mwandishi wa habari mmoja wa jarida la Sun akizungumzia alivyompiga mchezaji wa timu hasimu usoni katika ligi ya daraja la kwanza, ili apate kadi nyekundu na kisha baadaye alipwe pauni 70,000.

Alisema pia alipangia mchezaji mwingine aweze kulipwa pauni 30,000 kwa kupokea kadi ya njano katika mechi ya ligi. Klabu ya Portsmouth imeelezea kushtushwa sana na madai hayo.

Katika video hiyo liyorekodiwa kisiri, Sodje raia wa Nigeria, pia alidai ana uwezo wa kupanga mechi za ligi kuu na kuwa yuko tayari kupanga mechi katika kombe la dunia mwaka ujao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa klabu hiyo, alisema kuwa ikiwa madai haya ni ya kweli, basi ijulikane kuwa ni ya kushtua na kushangaza sana, jambo la kupanga mechi bila shaka linaathiri pakubwa maadili ya mchezo wa soka.


Sodje hachezei tena klabu ya Portsmouth lakini itambidi ashirikiane na maafisa wakuu kwa uchunguzi. Sodje aliondolewa uwanjani katika dakika ya 50 wakati wa mchuano kati ya Portsmouth na Oldham Athletic kwenye ligi ya daraja la kwanza 23 Februari mwaka 2013.
Read more
Jumapili, 8 Desemba 2013
KENYA WAWAPELEKA KILIMANJARO STARS MACHINJIONI KWENYE MATOPE

MECHI ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa Machakos.

Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa 64 kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10 mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja  na kituo cha televisheni cha SuperSport kupitia chaneli ya SS9.

Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Aga Khan katika Jiji la Mombasa.

Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars yalifungwa na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania nyavu ni Amri Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.


Read more
KIKWETE AMPONGEZA TENGA, AMBEBESHA ZIGO MALINZI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.

Ametoa changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.

Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.

Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.
Read more
PAMBANO LA TANZANITE LAINGIZA MIL 5/-

PAMBANO kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,732,012.01.

Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh. 6,190,000.


Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Read more
MAVETERANI MORO KUVAANA MWISHONI MWA WIKI HII

BONANZA la mchezo wa mpira wa miguu litakaloshirikisha timu mbalimbali za Veterani za mkoani Morogoro linatarajiwa kufanyika Desemba 14 na 15, mwaka huu, katika uwanja wa Shujaa, mjini hapa.

Akizungumza na mtandao huu, mratibu wa bonanza hilo, Daudi Julian alisema lengo la bonanza hilo, ni kuwakutanisha pamoja wanasoka wa zamani na kuimarisha afya zao.

Julian alisema maandalizi kuendelea bonanza hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa yanakwenda vizuri huku timu shiriki zikiwa katika mazoezi makali.

Mratibu huyo alizitaja baadhi ya timu zinazotarajia kushiriki katika bonanza hilo kuwa ni Moro Veterani, Reli Family Veterani, Kihonda Veterani, Mzumbe Veterani, Kichangani Veterani, Burkina Faso Veterani, Mazimbu Veterani na Shooting Stars Veterani.

“Maandalizi yanakwenda vizuri na tayari baadhi ya timu zimethibitisha kushiriki,” alisema.

Aidha, Julian alisema zawadi mbalimbali zinatarajiwa kutolewa kwa timu zitakazofanya vizuri ikiwemo pia zawadi kwa mchezaji mmoja mmoja.


“Hili bonanza ni la aina yake na kwamba halijawahi kufanyika mkoani Morogoro na niseme huu ni mwanzo tu, mabonanza zaidi yanakuja,” alisema.
Read more
Jumamosi, 30 Novemba 2013
 ZANZIBAR HEROES NJIA PANDA CHALENJI, YAKUBALI KIPIGO CHA 3-1 KUTOKA KWA ETHIOPIA

PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY BLOG

ZANZIBAR Heroes imejiweka njia panda kwenda au kutokwenda Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Chalenji baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Ethiopia mchana wa leo, Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.

Mabao yaliyoizamisha Zanzibar leo yalifungwa na nahodha, Fasika Asfan dakika ya tano, Salahadin Bargicho kwa penalti dakika ya 37 baada ya Manaye Fantu kuangushwa kwenye eneo la hatari wakati Yonathan Kebede alifunga la tatu dakika ya 83.

Bao la Zanzibar lilifungwa na kiungo mpya wa Simba SC, Awadh Juma Issa dakika ya 68 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Seif Abdallah Karihe, ambaye alimlamba chenga beki wa kulia wa Ethiopia kwanza.

Zanzibar ilipata pigo mapema tu dakika ya 14, baada ya mchezaji wake tegemeo Suleiman Kassim ‘Selembe’ kuumia nyama za paja na kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Seif Abdallah Karihe. 
 
Kwa kipigo cha leo, Zanzibar inabaki na pointi zake tatu ilizovuna kwa kuifunga Sudan Kusini 2-1 katika mchezo wa ufunguzi na Ethiopia iliyoanza kwa sare ya bila kufungana na wenyeji Kenya, inakuwa na pointi nne.



Read more
SALAMU ZA TFF KWENYE HAFLA YA KUPOKEA KOMBE HALISI LA DUNIA TANZANIA

Mheshimiwa Rais, nianze kwa kukushukuru kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe halisi la Dunia.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.

Coca-Cola ni washirika wetu wa karibu na wamekuwa wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu mwaka 2007, mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kuibua vipaji vingi ambapo baadhi yao wameweza kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.

Tunawashukuru sana Coca-Cola na tunaahidi  kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kuendeleza soka ya vijana.

Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba, 2009 wakati unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa kwa uongozi wa mpira wa Tanzania.

Ulitushauri tuimarishe uongozi na utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi klabu, ulitushauri tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha kufundisha timu zetu za mpira na pia ulitushauri tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka wakiwa na umri mdogo.

Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu tuliuzingatia na tulifanya jitihada za kuufanyia kazi. Hali ya utulivu katika uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale palipoonyesha dalili za migogoro tulikemea na ikibidi tulichukua hatua madhubuti kutatua migogoro.

Tumefanya kozi mbalimbali za kuwaendeleza walimu wetu wa mpira, waamuzi, madaktari na viongozi wetu wa ngazi mbalimbali na matokeo yake yanaonekana katika kuinuka kwa viwango vyao vya ufundishaji na utoaji uamuzi uwanjani.

Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza mwaka 2009 maendeleo ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya mpira kwa Taifa letu. Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28, Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa.

Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.

Fainali hizi uhusisha mataifa manane yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha timu mbili zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza fainali za dunia za vijana chini ya umri wa miaka 17.

Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine Babayaro na wengine kadhaa.

Ili tupate timu nzuri ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019.

Katika kuboresha kikosi hiki mwaka 2015 tutafanya mashindano ya kitaifa ya umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa ya umri chini ya miaka 14, 2017 yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na 2018 yatakuwa ya umri chini ya miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha mwisho cha kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.

Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020, kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.

Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013, Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Afrika umri chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019.

Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kanuni za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika haina budi ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi yake(Letter of support from Government).

Wiki ijayo tutawasilisha barua kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono na Serikali katika azma yetu hii, tunaomba Serikali ituunge mkono katika jambo hili.

Mheshimiwa Rais nimalizie kwa kukushukuru tena kwa uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wanaotupa katika shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa kutuwezesha kuwa moja ya nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili, Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa karibu.


Watanzania wenzangu ninaomba tuje kwa wingi kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuliona Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni kuwa ipo siku Kapteni wa Timu yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania kombe hili.
Read more
KOCHA WA CAMEROON ASAINI MIAKA MWILI AZAM

Kocha mpya wa Azam FC. Joseph Marius Omog (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

KLABU ya Azam inapenda kuufahamisha umma hususan wapenzi wa mpira wa miguu kuwa imeingia mkataba na kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia leo.

Kocha Omog ni bingwa kwani anakuja kuifundisha Azam akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013).

Timu hii ilikuwa haijatwaa ubingwa wa ligi kwa zaidi ya miaka 30. Kwa mwaka huu wametwaa ubingwa wakiwaacha wapinzani wao, Diables Noirs kwa pengo la pointi kumi (10) wakikusanya pointi 87 katika ligi yenye timu 18.

Pia ni mwaka jana tu (2012) aliiwezesha A.C Leopards kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.

Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika yalifikiwa baada ya miaka 38 tangu klabu ya Jamhuri yas Kongo ifanye hivyo, na kumfanya kocha Omog kuwa moja ya makocha wa kupigiwa mfano barani Afrika.

Kadhalika mwaka huu 2013, A.C Leopards chini ya ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Yote hayo ameyafanya akitumia asilimia kubwa ya wachezaji wa ndani ya Kongo huku akiwainua kutoka katika hali ya kuonekana wachezaji wa wastani hadi kuwa tishio na kuhofiwa kote barani Afrika.

Azam Football Club inamuona kocha Omog kuwa anakidhi vigezo vya kuendana na dira ya klabu ambayo ni kukuza na kuwaendeleza wachezaji na kushindana kwa kiwango cha juu kwa lengo la kuwa mabingwa katika mashindano mabalimbali ambayo timu inashiriki.

Uongozi wa Azam FC utampatia ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha malengo na mipango thabiti ya klabu.

Maelezo Binafsi
Kocha Omog ni mchezaji wa zamani wa timu ya Dragon Yaounde Cameroon. Alipata mafunzo ya ualimu wa michezo na elimu ya viungo (Sports and physical education) kutoka chuo cha vijana na michezo (Higher Institute of Youth and Sports, INJS Yaounde).

Baadaye alipata fursa ya kujiendeleza nchini Ujerumani ambako mwaka 1987 alitunukiwa stashahada ya ukufunzi wa mpira wa miguu na leseni B ya ukocha kwa viwango vya Shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya, UEFA.

Aliporejea nyumbani kwao Cameroon Joseph Marius Omog, alifundisha kabumbu katika klabu mbalimbali, zikiwemo; Fovu of Baham na Aigle of Menoua na kufanikiwa kufuzu kwa fainali za kombe la Cameroon. Mwaka 2001 aliteuliwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions chini ya kocha raia wa Ujerumani Winfried Schafer.


Omog amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Cameroon iliyoundwa na wachezaji wa ndani ijulikanayo kama Intermediate Lions hadi mwaka 2010 na baada ya hapo akelekea Kongo kuionoa A.C Leopards kwa mafanikio makubwa na hasa kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho wakiifunga Djoliba ya Mali kwa ushindi wa jumla wa magoli 4-3 katika michezo miwili ya fainali.
Read more
UMEWAHI KUIONA HII PICHA? RAGE AKIMALIZA BIASHARA YA OKWI

NDANI ya Simba sasa kumewaka moto kutokana na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo pamoja na wanachama ambao hawana imani na Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage hali iliyopeleka kutaka kumpindua mara mbili ndani ya mwaka huu.

Moja katika madai ambayo yanamtia matatani Rage ni kuuzwa kwa mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi kwa Etoile du Sahel ya Tunisia kwani hadi sasa fedha za kuuzwa mwanandinga huyo imekuwa ni kitendawili.

Pichani Rage anaonekana akipiga picha akipena mikono na mmoja wa viongozi wa Etoile du Sahel mara baada ya kumalizana biashara ya kuumza mshambuliaji huyo.



  
Read more
KOCHA WA AZAM ATUA LEO KUANZA KAZI

Joseph Marius Omog baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa JNIA kwa kazi ya kuifundisha Azam FC

KOCHA mpya wa timu ya Azam FC, Joseph Marius Omog amewasilia leo asubuhi tayari kwa kuifundisha timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho.

Kocha huyo raia wa Cameroon ambaye alikuwa akiifundisha timu ya AC Leopards ya Congo Brazzavile amewasili leo asubuhi akitokea kwao tayari kabisa kwa kuanza kibarua chake.

Kocha huyo mwenye mafanikio makubwa barani Afrika amekuja kuchukua nafasi ya Stewart Hall ambaye ametupiwa virago mara tu baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
Read more
Ijumaa, 29 Novemba 2013
FIFA WAFUNGUKA BAADA YA UWANJA WA KOMBE LA DUNIA KUPOROMOKA BRAZIL

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) imesema halina mpango wa kuhamisha michuano ya Fainali ya Kombe la Dunia 2014 kutoka nchini Brazil ingawa nchi hiyo imepata changamoto katika maandalizi ya michuano hiyo.

Wafanyakazi wawili walipoteza maisha baada ya kuangukiwa na nguzo ambazo ziliharibu uwanja wa Corithians ulio mjini Sao Paulo.

Timu ya taifa ya Brazil inatarajiwa kucheza mechi ya ufunguzi ya Kombe la dunia katika uwanja huo wenye uwezo wa kuwa na watazamaji 65,000.

Vyanzo vya habari vya juu ndani ya Shirikisho hilo vimeendelea kusisitiza kuwa hakuna mbadala kutokana na kutokea kwa ajali hiyo.

Brazil ilikiri kuwa inafanya jitihada za kumaliza ujenzi wa viwanja 12 kwa ajili ya michuano hiyo, sita kati ya hivyo ipo tayari kwa ajili ya michuano ya kombe la shirikisho.

Ajali iliyotokea siku ya Jumatano ni ya tatu kusababisha kifo katika viwanja vitakavyopigiwa kipute cha kombe la dunia. Wafanyakazi wengine wawili walipoteza maisha kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Uchunguzi umeanza hii leo kubaini chanzo cha ajali mjini Sao Paulo.
Read more
Alhamisi, 28 Novemba 2013
MAN UNITED YAWAPIGA WAJERUMANI 5-0, MAN CITY, MADRID ZAUA, BAYERN YAVUNJA REKODI YA BARCELONA

MANCHESTER United imefanya mauaji makubwa ugenini, baada ya kuitandika Bayer Leverkursen mabao 5-0 nchini Ujerumani katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.  

Mabao ya United yamefungwa na Valencia dakika ya 22, Spahic aliyejifunga dakika ya 30, Evans dakika ya 65, Smalling dakika ya 77 na Nani dakika 88. Wayne Rooney ndiye alikuwa nyota wa mchezo kutoka na kupika mabao manne katika ushindi huo ambao haukutarajiwa.  

Katika mchezo mwingine, winga Gareth Bale amewaongoza wachezaji 10 wa Real Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya Roberto Mancini, Galatasaray, akifunga bao tamu la mpira wa adhabu kipindi cha kwanza.

Huku Cristiano Ronaldo akiushuhudia mchezo huo kutoka jukwaa la VIP Uwanja wa Bernabeu, hakuna aliyeweza kumzuia Bale kufunga kwa mpira wa adhabu dakika ya 37.

Mabao mengine ya Real yalifungwa na Arbeloa dakika ya 51, Di Maria dakika ya 63 Isco dakika ya 80, wakati bao pekee la Galatasaray lilifungwa na Bulut dakika ya 38. 

Manchester City nao wameifumua mabao 4-2 Viktoria Plzen Uwanja wa Etihad katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mabao ya City yamefungwa na Aguero kwa penalti dakika ya 33, Nasri dkika ya 65, Negredo dakika ya 79 na Dzeko dakika ya 90, wakati mabao ya Viktoria Plzen yamefungwa na Horava dakika ya 43 na Tecl dakika ya 69. 

Jana usiku mabingwa watetezi, Bayern Munich wameendeleza ubabe katika Ligi ya Mabingwa baada ya kuicharaza mabao 3-1 CSKA Moscow Uwanja wa Khimki Arena katika mchezo wa Kundi D.

Mabao ya Bayern usiku huu yamefungwa na Arjen Robben, Mario Gotze na Thomas Muller kwa penalti. Huo unakuwa ushindi wa 10 mfululizo kwa Bayern na hivyo kuvunja rekodi ya mwaka 2002 ya Barcelona katika michuano hiyo.
  Winga wa Manchester United, Luis Nani akifunga bao la tano
   Wachezaji wa Manchester United wakishangilia nao la Johny Evans
   Kiungo wa Real Madrid, Sergio Ramos akitolewa kwa kadi nyekundu
   Mshambuliaji wa Galatasaray, Bulut akifunga bao pekee kwa timu yao
    Mshambuliaji wa Manchester City, Aguero akishangilia bao 








Read more
Jumatano, 27 Novemba 2013
ZANZIBAR MWENDO MDUNDO CHALENJI, YAICHAPA SUDAN KUSINI 2-1

ZANZIBAR imeanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Chalenji baada ya kuifuga mabao 2-1 Sudan Kusini katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi A, Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.

Mabao ya Zanzibar Heroes leo yalifungwa na kiungo wa Coastal Union ya Tanga, Suleiman Kassim ‘Selembe’ dakika ya saba baada ya kuipangua ngome ya Sudan Kusini na kufumua shuti lililomshinda kipa Juma Jinaro na Adeyoum Saleh Ahmed dakika ya 67.

Bao la Sudan Kusini lilifungwa na Fabiano Lako dakika ya 73, zikiwa ni dakika tano aiingie kuchukua nafasi ya Francis Khamis.

Zanzibar ingeweza kuondoka na ushindi mnene leo kama washambuliaji wake, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Ally Badru wangetumia vyema nafasi nzuri walizopata.

Nafasi nzuri zaidi ambayo Zanzibar walipata ilikuwa dakika ya 43 baada ya Badru kumlamba chenga kipa, lakini Khamis Mcha alipopiga mpira ukagonga mwamba na kipa akaudaka.

Zanzibar; Abdallah Rashid, Salum Khamis/Ally Khan dk78, Waziri Salum, Shaffi Hassan, Mohamed Fakhi, Sabri Ali, Masoud Ali, Suleiman Kassim, Awadh Juma na Khamis Mcha/Amour Omar dk44/Adeyoum Saleh dk62.


Sudan Kusini; Juma Jinaro, Atar Thomas, Philip Delfino, Edomon Amadeo, Richard Justin, Wiiam Offiri, Jimmy Erasto, Thomas Jacob, Godfrey Peter, Francis Khamis/Fabiano Lako dk68 na James Joseph.
Read more
ARSENAL YAUA 2-0, CHELSEA YAKALISHWA, BARCA NAYO CHALIIII, BALOTELLI AING'ARISHA AC MILAN

MABAO mawili ya kiungo Jack Wilshere leo yameipa ushindi wa 2-0 Arsenal dhidi ya Marseille ya Ufaransa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku huu Uwanja wa Emirates.

Ilimchukua sekunde 29 tangu kuanza kwa mchezo huo kiungo huyowa England kufunga bao la kwanza akimtungua kipa hodari, Steve Mandanda na akfunga tena bao la pili dakika ya 65. 

Nayo Barcelona jana ilionja joto ya jiwe baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ajex katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mjini Amsterdam. Pamoja na ushindi huo, Ajax ilimaliza pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Veltman kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 48.

Mabao ya Ajax yalifungwa na Serero dakika ya 18 na Hoesen dakika ya 41 kabla ya Xavi kuifungia Barca bao la kufutia machozi kwa penalti dakika ya 49.
 

Katika mchezo mwingine, Chelsea imefungwa bao 1-0 na FC Basle, bao pekee la Mohamed Salah. Mabao ya Kaka dakika ya 12, Zapata dakika ya 49 na Balotelli dakika ya 59 yameipa AC Milan ushindi wa 3-0 dhidi ya Celtic nchini Scotland katika mchezo mwingine wa michuano hiyo. 






Read more