MABAO matatu ya kusawazisha ya Simba katika mchezo wa
watani wa jadi, juzi yamezidi kuitesa Yanga baada ya jana badala ya kuanza
mazoezi kujiandaa na mchezo wa kesho walikaa kujadili sababu za kutoka sare
katika mchezo huo.
Yanga katika mchezo huo, walitawala mchezo kwa
dakika 45 za kwanza na kuwasaidia kupata ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na
Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza aliyefunga mawili kabla ya Simba kusawazisha
katika kipindi cha pili.
Simba ambao waliingia vyumbani wakiwa tayari
wamelala kwa mabao hayo matatu, lakini walirudi kwa kasi na kufanikiwa
kusawazisha mabao yote matatu na kufanya mchezo huo umalizike kwa matokeo ya
sare.
Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts jana aliwakarisha
chini wachezaji wake na kuwataka mmoja baada ya mwingine aeleze sababu ya
mchezo huo kumalizika kwa sare wakati wao wakiwa wameshamaliza mchezo huo
katika kipindi cha kwanza.
Brandts alimtaka mchezaji mmoja mmoja aeleze kile
anachokijua kwanini wameshindwa kushinda katika mchezo huo na ndipo wachezaji
hao walipoanza kufunguka.
Lakini baadhi ya wachezaji wakiwemo Jerry Tegete na
Didier Kavumbagu waliumtaka kocha wao waache kujadili kwani hakuna sababu ya
kufanya hivyo kwa kuwa sababu ya kutoka sare ni uzembe ya baadhi ya wachezaji
wenzao.
Pamoja na maombi hayo ya Tegete na Kavumbagu lakini
Brandts aliwataka waendelee kutoa maoni yao na baada ya kumaliza ndipo mazoezi
yaliendelea.
Kesho Yanga itavaana na Rhino Rangers mchezo
utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Simba watakuwa mjini
Tanga kupepetana na Coastal Union.
0 comments