Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi
KLABU ya soka ya Barcelona inasubiri ripoti ya
madaktari kuona kama mshambuliaji wao, Lionel Messi, ambaye anahofiwa kuwa
atakuwa na tatizo katika misuli ya paja baada ya kulazimika kutolewa wakati wa
mapumziko katika mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Atletico Madrid.
Bao la kwanza kwa Neymar akiwa Camp Nou lilizima lile
walilofungwa mapema na mshambuliaji wao wa zamani, David Villa, ukiwa ni mchezo
wa kwanza wa michuano ya Super Cup uliopigwa jana usiku, lakini kutolewa kwa
Messi kuliwafanya wageni kupata nguvu zaidi.
"Messi alilazimika kutolewa baada ya
kulalamikia misuli ya paja lake la kushoto," ilisomeka taarifa iliyokuwa
katika mtandao wa klabu hiyo wakati mchezo ukikaribia kumalizika.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina
anatarajiwa kufanyiwa vipimo leo mchana ili kupata majibu ya tatizo lake, huku
akiacha wasiwasi kwa timu yake kama tatizo alilopata linafanana na lile
lililomfanya kushindwa kumaliza msimu uliopita vizuri.
Messi alipata maumivu kama hayo katika mchezo wa
kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris Saint-Germain.
Na mchezo uliofuata aliingia akitokea benchi na
kuisaidia Barca kupata ushindi, lakini nyota huyo mwenye miaka 26 aliumia tena
na kuacha michezo mitatu ya mwisho ya La Liga wakati timu yake ikiwa tayari imetwaa
ubingwa.
0 comments