WATU watatu wanashikiliwa na polisi nchini England
baada ya aliyekuwa mchezaji wa Portsmouth kumwambia mwandishi wa habari kuwa
alihusika katika kupanga mechi.
Sam Sodje alirekodiwa kwenye kanda ya video na
mwandishi wa habari mmoja wa jarida la Sun akizungumzia alivyompiga mchezaji wa
timu hasimu usoni katika ligi ya daraja la kwanza, ili apate kadi nyekundu na
kisha baadaye alipwe pauni 70,000.
Alisema pia alipangia mchezaji mwingine aweze
kulipwa pauni 30,000 kwa kupokea kadi ya njano katika mechi ya ligi. Klabu ya
Portsmouth imeelezea kushtushwa sana na madai hayo.
Katika video hiyo liyorekodiwa kisiri, Sodje raia wa
Nigeria, pia alidai ana uwezo wa kupanga mechi za ligi kuu na kuwa yuko tayari
kupanga mechi katika kombe la dunia mwaka ujao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa
klabu hiyo, alisema kuwa ikiwa madai haya ni ya kweli, basi ijulikane kuwa ni
ya kushtua na kushangaza sana, jambo la kupanga mechi bila shaka linaathiri
pakubwa maadili ya mchezo wa soka.
Sodje hachezei tena klabu ya Portsmouth lakini
itambidi ashirikiane na maafisa wakuu kwa uchunguzi. Sodje aliondolewa uwanjani
katika dakika ya 50 wakati wa mchuano kati ya Portsmouth na Oldham Athletic
kwenye ligi ya daraja la kwanza 23 Februari mwaka 2013.
0 comments