TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imeshindwa
kuvuruga sherehe za Uhuru wa Kenya ambapo kilele chake kinafanyika Desemba 12
ambayo ndiyo siku ya fainali ya Kombe la Challenge.
Kilimanjaro Stars kama ingeifunga Kenya katika hatua
ya nusu fainali ya leo usiku, timu hiyo isingeweza kucheza fainali na kutwaa
kombe katika sherehe za kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Kenya.
Kili Stars imekubali kipigo cha bao 1-0 na Kenya
‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na
Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, usiku huu ikisindikizwa na
mvua.
Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia
katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu keshokutwa mchana Uwanja wa Nyayo tena,
wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.
Mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbwana Samatta
akiwatoka mabeki wa Kenya, Joackins Atudo kulia na Aboud Omar kushoto Nyayo
usiku huu.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Thiery
Nkurunziza wa Burundi, aliyesaidiwa na Idam Hamid wa Sudan na Mussie Kinde wa
Ethiopia, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0,
lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya
nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na
kumchungulia kipa Ivo Mapunda.
Baada ya bao hilo, Stars walizinduka na kuanza
kushambulia, lakini ukuta wa Kenya ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote.
Nafasi pekee nzuri ambayo Stars waliipata ilikuwa
dakika ya 44, wakati kona nzuri ya Mrisho Ngassa ilipopanguliwa na kipa Duncan
Ochieng, lakini Mbwana Samatta akachelewa kuunganisha, Joackins Atudo
akaondosha kwenye hatari.
Kipindi cha Stars ilicheza vizuri zaidi, lakini bado
ukuta wa Harambee ulikuwa mgumu na nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho
ilikuwa dakika ya 88, wakati Mbwana Samatta alipomtoka beki wa Kenya na kuingia
vizuri ndani ya 18, lakini akapiga juu.
Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa
wakilia na ikabidi viongozi wachukue jukumu la kuwabembeleza. Nahidha Kevin
Yondan ndiye alikuwa ana hali mbaya zaidi.
0 comments