PAMBANO kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini
(Basetsana) lililochezwa jana (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam limeingiza sh. 5,353,000.
Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya
raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The
Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh.
2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh.
1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa
uwanja walipata sh. 433,003.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata
sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh.
1,732,012.01.
Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji
iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao
10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh. 6,190,000.
Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba
20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
0 comments