NEYMAR APIGA HAT TRICK YA KWANZA ULAYA BARCA IKIUA 6-1, ARSENAL YAPENYEA TUNDU LA SINDANO 16 BORA
KLABU ya Barcelona jana iliingia hatua ya 16 Bora
kwa kishindo baada ya kuitandika Celtics mabao 6-1 huku mshambuliaji wake
wa Brazil, Neymar akipiga hat-trick yake
ya kwanza barani Ulaya.
Licha ya Barcelona kuwakosa Andres Iniesta aliyebaki
benchi, Leonel Messi ambaye bado majeruhi na Cesc Fabregas anayetumikia adhabu,
imeendeleza makali yake ya kutoa kichapo hicho cha mbwa mwizi.
Neymar aliyeongoza safu ya ushambuliaji hakufanya
makosa baada ya kufunga hat trick yake ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa dakika
za 45, 48 na 58, wakati mabao mengine yalifungwa na Pique dakika ya saba, Pedro
dakika ya 39, na Tello dakika ya 72.
Kwa upande wa Arsenal wao wameponea chupuchupu
kukosa hatua ya 16 bora baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa
Napoli ya Italia na kufanya timu zote tatu za kundi F zikifungana kwa pointi
baada ya kumaliza wakiwa na pointi 12 na mabao ndiyo yaliyoipeleka hatua ya
mtoano.
Arsenal ambayo walimaliza mchezo huyo wakiwa pungufu
baada ya dakika ya 76, nahodha wake, Mikel Arteta alipotolewa nje kwa kadi
nyekundu hali iliyosababisha kuleta udhaifu katika kikosi cha Arsene Wenger.
Mabao ya Napoli yamefungwa na Gonzalo Higuain dakika
ya 73 Callejon dakika ya 90.
Katika mchezo mwingine, timu ya Chelsea ilifanikiwa
kuibuka na ushindi wa bao 1-0 bao pekee lilofungwa na Demba Ba dakika ya 11,
limempa faraja kocha Jose Mourinho wa Chelsea kwa ushindi huo dhidi ya Steaua
Bucharest.
Mapema mchana wa jana katika mchezo wa kiporo, bao
pekee la Wesley Sneijder liliipa ushindi wa 1-0 nyumbani Galatasaray dhidi ya
Juventus na kufuzu 16 Bora, huku Kibibi Kizee cha Turin kikifungishwa virago.
Katika mechi nyingine za usiku huu, Marseille
imefungwa 2-1 nyumbani na Borussia Dortmund, Atletico de Madrid imeidunga 2 - 0
FC Porto, FC Schalke 04 imeifunga 2 - 0 Basel, FK Austria Wien imeifunga 4-1
Zenit St Petersburg, AC Milan imetoka sare ya
0-0 na Ajax.