Open top menu
Jumatatu, 25 Novemba 2013
CHUJI, CANNAVARO, YONDANI, MSUVA,TEGETE WAJIFUNGA YANGA, SASA KUKIPIGA HADI 2016

WACHEZAJI watano wa timu ya Yanga wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.

Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Yanga ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016).

Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Yanga, Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.

"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.


Wakati huo huo kikosi cha Yanga leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Read more
KILIMANJARO STARS YAENDA NAIROBI NA MATUMAINI KIBAO

TIMU ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ imeondoka kuelekea nchini Kenya kwa mashindano ya kombe la chalenji linalotaraji kuanza kuunguruma November 27.


Kilimanjaro Starz imeondoka na matumaini kibao ya kurejea na kikombe hicho kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).

Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.



Read more
Jumamosi, 23 Novemba 2013
TFF YAMRUDISHA RAGE SIMBA, YAMPA MASHARTI MAGUMU

MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage ameagizwa kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia sasa.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.

Kwa maagizo hayo kutoka TFF kwenda kwa Rage ina maanisha kuwa shirikisho hilo limetambua nafasi yake kama mwenyekiti na kutupilia mbali barua ya Kamati ya Utendaji ya Simba iliyomsimamisha.

TFF kama ingetambua barua ya Kamati ya Utendaji ya Simba basi angepewa maagizo Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi' kuitisha mkutano huo badala ya Rage aliyesimamishwa.

Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”


TFF itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.
Read more
MALINZI AMRUDISHA MWAKALEBELA TFF, WAPO PIA NASSIB NA MADEGA

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametangaza wajumbe wa kamati ndogondogo wakiwemo Katibu Mkuu wa zamani, Fredrick Mwakalebela na Makamu wa pili wa TFF aliyemaliza muda wake, Ramadhani Nassib (standing committees) wakati zile za haki (judicial organs) na uchaguzi zitaundwa baadaye.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika leo (Novemba 23 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi alisema kamati hizo zimeundwa kwa mujibu wa katiba ili kuisaidia Kamati ya Utendaji.

Pia ametangaza wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji aliowateua. Wajumbe hao ni Richard Sinamtwa na Ramadhan Nassib, wakati wengine wanaoingia moja kwa moja kwenye Kamati ya Utendaji kutokana na kamati wanazoziongoza ni Dk. Paul Marealle na Saloum Umande Chama.

Kamati ya Fedha na Mipango inaongozwa na Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wajumbe ni Francis Ndulane (Makamu Mwenyekiti), Omari Walii, Eliud Mvella, Said Muhammed, Geofrey Nyange, Kidao Wilfred, Ayoub Nyenzi, Lina Kessy na Cyprian Kuhyava.

Geofrey Nyange anaongoza Kamati ya Mashindano wakati wajumbe ni Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti), Msafiri Mgoyi, James Mhagama, Mohamed Nassoro, Moses Katabaro, Seif Ahmed, Gerald ambi, Davis Mosha, Said George na Nassoro Idrissa.

Kinara wa Kamati ya Ufundi ni Kidao Wilfred wakati wajumbe ni Athumani Kambi (Makamu Mwenyekiti), Vedstus Lufano, Blassy Kiondo, Rahim Kangezi, Patrick Kahemele, Daud Yassin, Nicholas Mihayo na Dk. Cyprian Maro.

Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana inaongozwa na Ayoub Nyenzi, Khalid Abdallah (Makamu Mwenyekiti), Ali Mayay, Mulamu Ng’hambi, Apollo Kayungi, Said Tully, Luteni Kanali Charles Mbuge, Lameck Nyambaya na Ibrahim Masoud.

Lina Kessy anaongoza Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake wakati wajumbe ni Shyrose Bhanji (Makamu Mwenyekiti), Zena Chande, Amima Karuma, Dk. Cecilia Makafu, Zafarani Damoder, Beatrice Mgaya, Sofia Tigalyoma, Martin Mung’ong’o na Engrid Kimaro.

Kamati ya Waamuzi inaongozwa na Saloum Umande Chama, Nassoro Said (Makamu Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu), Riziki Majala, Kanali Isaro Chacha, Paschal Chiganga, Victor Mwandike, Soud Abdi na Zahra Mohamed.

Hamad Yahya Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi anaongoza Kamati ya Habari na Masoko wakati wajumbe ni Naibu Waziri January Makamba (Makamu Mwenyekiti), Tido Mhando, Yusuf Manji, Yusuf Bakhresa, Samwel Nyalla, Jack Gotham, Fredrick Mwakalebela na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inaongozwa na Richard Sinaitwa, Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.

Kiongozi wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha ni Ramadhan Nassib wakati wajumbe ni Zitto Kabwe (Makamu Mwenyekiti), Nicholas Magarinza, Jackson Songora, Epaphra Swai, Kalilo Samson, Goodluck Moshi, Golden Sanga na Elias Mwanjala.


Dk. Paul Marealle anaongoza Kamati ya Tiba wakati wajumbe ni Dk. Fred Limbanga (Makamu Mwenyekiti), Dk. Mwanandi Mwankemwa, Dk. Nassoro Matuzya, Dk. Eliezer Ndelema na Asha Sadick.
Read more
MTANZANIA WA KWANZA KUWANIA TAJI LA DUNIA LA WBC

BONDIA Mtanzania Omari Kimweri  'Lion Boy' anayefanya shughuli zake Deer Park, Victoria, nchini Australia anatarajia kuwa mtanzania wa kwanza kupanda ulingoni  Novemba 30, mwaka huu  kugombea ubingwa wa Dunia unaotambuliwa na  WBC uzito wa kg 47.5.

Mpambano huo utakaopigwa nchini ya China na bingwa wa dunia wa uzito huo nchini humo, Xiong Zhao Zhong ambaye ndiye anayeshikilia taji hilo la ubingwa wa dunia WBC.

Kimweri anakuwa mtanzania wa kwanza kuwania taji kubwa kabisa duniani akitokea nchini Austalia huku sapoti kubwa akitegemea kutoka Tanzani ambapo alipozaliwa. 

Kigezo cha kufanya apate pambano hilo kubwa ni kutokana na rekodi yake pamoja na kutakiwa bondia mwenye asili ya Afrika ambapo kula imemdondokea Kimweri kwa mara ya kwanza mtanzania huyo ataonekana Dunia nzima akijaribu kuwania ubingwa wa WBC.


Kimweri kwa sasa yupo katika mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mpambano huo amesema kuwa yeye binafsi yupo tayari kabisa kwa mpambano huo, amewaomba Watanzania waendelee kumuombea kwani maombi hayo yatamsaidia kunyakua taji hilo.
Read more
Alhamisi, 21 Novemba 2013
FIFA YAMSAFISHIA NJIA RONALDO KUTWAA TUZO YA BALLON D’OR 2013

KITENDO cha Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa) kutangaza kuongeza muda wa kupiga kura za kumchaguza mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d’Or 2013 kutoka Novemba 15 hadi Novemba 29 kimekuwa na faida kubwa kwa Cristiano Ronaldo.

Maamuzi hayo yametafsiriwa ni kama ya kumbeba Cristiano Ronaldo dhidi ya wapinzani wake kama Lionel Messi, Franck Ribery na Zlatan Ibrahimovic, baada ya nahodha huyo wa Ureno kupiga hat trick dhidi ya Sweden na kuipa tiketi timu yake ya Taifa kukata tiketi ya fainali za kombe la dunia 2014.


Mwisho wa makocha, manahodha na waandishi wanaopiga kura hizo kuwasilisha majina matatu ya juu ilikuwa November 15, saa kadhaa baada ya kumalizika kwa michezo ya hatua ya mtoano na Rebery anayecheza Bayern Munich alikuwa akipewa nafasi zaidi ya kuibuka na ushindi wa tuzo hiyo.
Read more
KIM POULSEN AMEFIKIA KIKOMO CHAKE

Na Erasto Stanslaus               
KIM Poulsen, Kocha mkuu wa Taifa Stars aliyejijengea umaarufu kwa kutengeneza kikosi kamambe cha ushindi, sasa anasumbuliwa na Matokeo Makubwa Sasa.

Mipango yake ni ya dharura. Kocha huyo aliyekuwa anategemea timu za vijana za Ngorongoro Heroes (U-20) na Serengeti Boys (U-17) kama vitalu vya kupata wachezaji wa baadaye wa Stars amebadilika ghafla na kubaki akitegemea wakongwe.

Mfano, katika uteuzi wa Stars hivi karibuni Kim aliamua kutengeneza kundi jipya lisilo na daraja akaliita Future Young Stars yaani Nyota wa Stars ya Baadaye.

Kundi hilo la Future Young Stars ni la akina Aishi Manula, Hussein Shariff, Ivo Mapunda, David Luhende, Hassan Mwasapili, Himid Mao, Issa Rashid, Ismail Gambo, John Kabanda, Kessy Khamis, Michael Pius, Miraji Adam, Mohamed Hussein, Said Moradi na Waziri Salum.

Wengine ni Amri Kiemba, Farid Mussa, Haruni Chanongo, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, Simon Msuva, William Lucian, Elias Maguli, Hussein Javu, Joseph Kimwaga, Juma Liuzio, Mwagane Yeya na Paul Nonga.

Lakini aliowaita kuunda Taifa Stars ni Ally Mustafa, Mwadini Ali, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Shomari Kapombe, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Vincent Barnabas, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Athuman Idd, Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samata na John Bocco.

Wachezaji 16 kutoka Future Young Taifa Stars wameungana na 16 wa Taifa Stars kuunda timu kamili ambayo ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe na kutoka suluhu. Stars ilielemewa sana hasa kipindi cha pili na mashabiki wa Stars hawakuridhishwa na kiwango cha kikosi hicho hivyo walipandwa na hasira na kuanza kumzomea Kim mara baada ya mchezo kumalizika.

Tujiulize, Ivo Mapunda aliyeichezea Stars akaachwa kwa madai kiwango kimeshuka nafasi yake ikatwaliwa na Juma Kaseja bado leo tunaambiwa ni Future Young Taifa Stars?

Umri wa Amri Kiemba ambaye leo anaitwa matumaini ya baadaye ni mkubwa kuliko Frank Domayo au Aboubakar Salum ambao ni matumaini ya sasa. Nani alipaswa kuwa matumaini ya  baadaye kati ya wachezaji hao?

Inawezekanaje Said Morad na Hussein Javu wawe matumaini ya baadaye wakati Thomas Ulimwengu na Shomari Kapombe ni mategemeo ya sasa?

Hapa ni wazi kuwa Kim ama amefikia ukomo wa ujuzi wake au anataka Matokeo Makubwa Sasa. Anataka timu ya kushinda michezo sasa na siyo hicho kiitwacho Future Young Taifa Stars.

Kwa mfumo anaoutumia Kim kuwategemea vijeba zaidi kuliko vijana ni ngumu kupata mafanikio yenye mwendelezo. Inawezekana timu ikaonekana ‘bora’ sasa lakini ikapotea kabisa katika ramani ya soka.

Kama kweli Kim angekuwa na nia ya kweli ya kuiboresha Stars baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani na zile za Afrika, ulikuwa muda muafaka wa kutengeneza kikosi cha baadaye cha Stars kwa kuwatumia wachezaji vijana wa Serengeti na Ngorongoro.

Hii inaonesha kuwa hakuna mipango ya kufanya vizuri kwa miaka ya baadaye kwani mfumo huu unawapoteza wachezaji vijana na kuwabeba vijeba ambao safari yao kisoka imefikia tamati.


MAKALA IMETOKA GAZETI LA MAWIO
Read more
SIMBA YAZIDI KUJIVURUGA YENYEWE

Na Erasto Stanslaus
SIMBA ya Dar es Salaam imeanza kufuata nyayo za msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Bara zilizoifanya ianze vizuri lakini ikaishia kushika nafasi ya tatu.

Klabu hiyo ilianza msimu ikiwa na kocha Milovan Cirkovic lakini katikati ya msimu ikamtimua na nafasi yake ikachukuliwa na Mfaransa, Patrick Liewig aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu.

Msimu huu, Simba ilianza kunolewa na Abdallah Kibaden akisaidiwa na Jamhuri Kihwelu ambao wametupiwa virago. Taarifa zinasema kwamba ataajiriwa Zdravko Logarusic wa Croatia aliyewahi kuifundisha Gor Mahia ya Kenya.

Katikati ya msimu uliopita Simba, uliibuka mgogoro wa uongozi ambao ulipelekea baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu. Msimu huu Kamati ya Utendaji imemsimamisha Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.

Sababu za kusimamishwa kwake ni danadana kuhusiana na ziliko fedha za uuzwaji wa mchezaji wao Emmanuel Okwi pamoja na kutojishughulisha sana na masuala ya klabu. Okwi aliuzwa katika klabu ya Étoile du Sahel ya Tunisia kwa dola 300 (Sh. 480 milioni).

Rage ndiye alifanya mazungumzo na Étoile na ndiye aliyekamilisha dili la kumuuza lakini fedha hizo hazikufika klabuni. Fedha hizo ndiyo sababu ya kukorofishana na tawi la Mpira Pesa.


MAKALA IMETOKA GAZETI LA MAWIO
Read more
KIM ATAJA ASKARI 23 KOMBE LA CHALENJI, IVO, SAMATA, ULIMWENGU NDANI

KOCHA Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 mwaka huu.

Kilimanjaro Stars iliyotwaa kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya Kocha Jan Poulsen, na ambayo imepangwa kundi B katika michuano ya mwaka huu itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.

Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Tanzania Bara ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).


Kilimanjaro Stars inatarajia kuondoka Jumatatu (Novemba 25 mwaka huu) kwenda Nairobi kushiriki michuano hiyo itakayoanza Novemba 27 mwaka huu na kumalizika Desemba 13 mwaka huu.   
Read more
MECHI DHIDI YA STARS, ZIMBABWE YAINGIZA MIL 50/-

MECHI ya kirafiki ya kimataifa ya FIFA Date kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (The Warriors) iliyochezwa juzi (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 50,980,000 kutokana na watazamaji 7,952.

Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 7,776,610.17 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 3,682,560.

Asilimia 15 ya uwanja sh. 5,928,124, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 7,904,166 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,976,041.

Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 17,784,373 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 889,219 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
Read more