Shaffih Kajuna Dauda ameenguliwa katika uchaguzi huo
Kamati ya Uchaguzi imepitisha majina ya
waombaji 40 kati ya 58 kwa ajili ya uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utakaofanyika mwezi ujao.
Waliopitishwa katika orodha hiyo ya
awali kwa upande wa Bodi ya Ligi ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said
Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti).
Kwa upande wa Kamati ya Uendeshaji
(Management Committee) ni Kazimoto Miraji Muzo na Omar Khatib Mwindadi.
Walioondolewa kwa vile si wenyeviti wa klabu za daraja la kwanza kama kanuni
zinavyotaka ni Michael Njuweni Kaijage, Salum Seif Rupia na Silas Masui
Magunguma.
Kanda namba moja (Kagera na Geita)
aliyepitishwa kuwania nafasi ya ujumbe Kamati ya Utendaji ya TFF ni Kaliro
Samson wakati Abdallah Hussein Musa ameondolewa kwa kutojaza fomu ya uchaguzi
kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
Jumbe Oddessa Magati, Mugisha Galibona
na Vedastus Lufano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba mbili (Mara
na Mwanza). Samwel Nyalla ameondolewa kwa kutojaza kikamilifu fomu namba 1 ya
maombi ya kugombea uongozi wa TFF kwa kutoonesha malengo yake.
Waliopitishwa katika Kanda namba tatu
(Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Swain a Mbasha Matutu wakati Stanslaus Nyongo
ameondolewa kwa kukosa sifa ya uongozi wa angalau uzoefu wa miaka mitano kwa
mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.
Kanda namba nne (Arusha na Manyara)
wamepitishwa wote watatu; ambao ni Ali Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omar Walii
Ali. Kanda namba tano (Tabora na Kigoma) nao wamepitishwa wote; Ahmed Idd Mgoyi
na Yusuf Hamis Kitumbo.
Blassy Kiondo amepitishwa peke yake
kuwania ujumbe Kanda namba sita (Katavi na Rukwa) huku Ayoub Nyaulingo
aliondolewa kwa kutokuwa na uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi
wa mpira wa miguu.
Athuman Nyamlani mgombea wa nafasi ya Rais
Naye Nazarius Kilungeja, Kamati ilikataa
maombi yake ya kugombea ujumbe kutokana na vitendo vyake visivyo vya kimichezo
ambavyo kwa kiasi kikubwa vilisababisha migogoro kwenye Mkoa wa Rukwa, hivyo
suala lake litawasilishwa kwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Kanda namba saba (Iringa na Mbeya)
waliopitishwa ni David Samson Lugenge, John Exavery Kiteve na Lusekelo Elias
Mwanjala. Cyprian Kuyava hakupitishwa kwa vile hana uzoefu wa uongozi kwa
mujibu wa Katiba ya TFF huku Ayoub Shaib Nyenzi akiondolewa kwa kushindwa
kuthibitisha uraia wake.
Elliud Peter Mvella ameondolewa kwa
kushindwa kuheshimu Kanuni za Uwajibikaji wa Pamoja (collective responsibility)
baada ya kushiriki kufanya uamuzi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF bila ya
kutaka msimamo wake wa kupinga uwekwe kwenye muhtasari na baadaye kuupinga
uamuzi huo akiwa kwenye uongozi wa mkoa. Suala lake limewasilishwa katika
Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Waliopitishwa kuwania ujumbe kupitia
Kanda namba nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick Mhagama na Stanley William
Lugenge wakati Kamanga Tambwe ameondolewa kwa vile alipatikana na hatia ya
kushiriki kwenye tuhumu za rushwa kwa waamuzi na kufungiwa na TFF.
Jamal Malinzi mgombea wa nafasi ya Rais
Kanda namba tisa (Lindi na Mtwara)
waombaji wote watatu wameptishwa. Waombaji hao ni Athuman Kingome Kambi,
Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder. Pia waombaji wote wa Kanda
namba kumi (Dodoma na Singida), Hussein Zuberi Mwamba, Stewart Ernest Masima na
Charles Komba wamepitishwa.
Waombaji wanne kati ya watano
wamepitishwa kwa Kanda namba 11 (Morogoro na Pwani). Waliopitishwa ni Farid
Mbarak, Geofrey Nyange, Juma Abbas Pinto na Twahil Twaha Njoki.
Riziki Juma Majala ameondolewa kwa vile
akiwa mtendaji mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA)
alishindwa kusimamia Kanuni za Ligi kwa kuruhusu timu ambayo si mwanachama wa
wanachama wa COREFA kucheza ligi, hivyo kusababisha mgogoro mkubwa kiasi cha
mwananchi mmoja kufungua kesi ya kusimamisha Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).
Suala lake litawasilishwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Kanda namba 12 (Kilimanjaro na Tanga)
wamepitishwa waombaji wote wawili. Waombaji hao ni Davis Elisa Mosha na Khalid
Abdallah Mohamed. Waombaji wawili kati
ya watano wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 13 (Dar es Salaam).
Wagombea wawili kati ya watano
wamepitishwa kuwania ujumbe kupitia Kanda namba 13 (Dar es Salaam). Wagombea hao ni Alex Crispine Kamuzelya na
Muhsin Said Balhabou.
Walioondolewa ni Omar Isaack Abdulkadir
kutokana na vitendo vyake vya kutoheshimu na kutotekeleza maagizo ya TFF kwa
mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF. Atapelekwa katika Kamati ya
Maadili kwa hatua zaidi.
Shaffii Kajuna Dauda ameondolewa kwa
kutumia nyaraka ya mawasiliano baina ya FIFA na Rais wa TFF bila idhini na
kuiweka hadharani kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, hivyo kukiuka
maadili kwa kumiliki nyaraka ambazo hazikuwa kwenye mamlaka yake. Suala lake
linapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Naye Wilfred Kidao ameondolewa kwa
kutumia nyaraka za Kamati ya Utendaji ya TFF bila ridhaa ya kamati, hivyo
kukosa uadilifu. Suala lake linawasilishwa kwenye Kamati ya Maadili kwa hatua
zaidi.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu wa Rais,
waombaji wote watatu wamepitishwa. Waombaji hao ni Imani Omari Madega, Ramadhan
Omari Nassib na Wallace John Karia.
Iman Madega mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais
Athuman Jumanne Nyamlani na Jamal Emil
Malinzi wamepitishwa kuwania nafasi ya Rais. Omari Mussa Nkwaruro ameondolewa
kwa kuwasilisha cheti chenye utata, hivyo kukiuka utashi wa Ibara ya 27(7) ya
Katiba ya TFF. Pia aliwasilisha taarifa za uongo kuhusu uzoefu na kukiuka
Kanuni za Maadili, hivyo suala lake linapelekwa Kamati ya Maadili.
Naye Richard Julius Rukambula
ameondolewa kwa hakukidhi matakwa ya kugombea uongozi kwa mujibu wa Ibara ya
12(2)(e) ya Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kupelekwa
katika mahakama za kawaida. Hivyo naye anapelekwa katika Kamati ya Maadili kwa
hatua stahiki.
0 comments