RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu
ilipokabidhi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.
Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa
lengo la kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo
limeleta mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa
na makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja
kwenye Kamati ya Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani
tumeanzisha jambo hili kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema
Rais Tenga wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali
vya habari.
Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala
bora watu wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa
kampuni kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.
Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika
ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo
yenye udhamini mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya
televisheni.
Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za
Ligi Kuu hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti
zao za mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika
zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema
bado linafanyiwa kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko
katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka
iwezekanavyo.
“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu
ambazo haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika
karibu viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za
kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system
(mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia uwezekano
wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa una system yake
tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala lisitucheleweshe,” amesema.
0 comments