KOCHA Brendan Rodgers ameliambia gazeti la Guardian
la England kuwa hahofii kumtumia Luis Suarez katika kikosi cha Liverpool
kinachokipiga na Manchester United leo katika mchezo wa kwanza wa Capital One
Cup.
Suarez yuko katika listi ya Rodgers tena baada ya
kufungiwa michezo 10, huku akiukosa mchezo wa kichapo cha bao 1-0 walichokipta
mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Southampton, kifungo alichokipata baada ya
kumng'ata kwa makusudi beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic, msimu uliopita.
Na anatarajiwa kurudi katika mchezo huo unaopigwa
leo kwenye Uwanja wa Old Trafford, wakati mchezaji huyo pia akikumbukwa kwa
kufungiwa michezo nane kwa kumtolea lugha ya kibaguzi beki wa United, Patrice
Evra 2011.
Rodgers anaamini kuwa Suarez atakuwa tayari kupokea
mapokezi mabaya Old Trafford. Na alisema: "Sihofii chochote juu ya
kumpanga Luis. Tangu nimekuwa hapa sikuwahi kukutana na kitu kama hicho. Kuna
historia katika michezo hii lakini sielekezi akili yangu huko.
"Luis ni mchezaji mwenye jina kubwa. Na ni
mmoja kati ya wachezaji wakubwa wenye matukio ambaye nimewahi kukutana naye
katika maisha yangu. Sidhani kama mapokezi yatamchanganya.
"Ni mpiganaji na malengo yake ya kufanikiwa
yapo kwa ajili ya kila mmoja kumuona. Tunafurahikuona kuwa amerudi kikosini.
Najua hata wachezaji wana furaha kurudi kwa mchezaji huyu uwanjani kutokana na
ubora wake."
Rodgers aliongeza: "Sidhani kama atakuwa katika
ulinzi mkubwa kama ambavyo imekuwa katika michezo iliyopita. Luis ni aina hiyo
ya mchezaji. Siku zote huzungumza anapochezewa vibaya. Kazi anayofanya
anapokuwa ndani na karibu na eneo la hatari huwafanya mabeki kuwa katika wakati
mgumu.
"Ni sehemu ya mchezo na unatakiwa kuendana
nayo. Nafikiri huu ni mchezo mzuri kwetu baada ya kutoka vichwa chgini katika
mchezo uliopita dhidi ya Southampton. Luis atakuwa sehemu ya mchezo huu.
"Nina uhakika kuwa wakati Luis atakapojua kuwa
ni sehemu ya mchezo huu, itamshitua na kumfanya kuwa tayari kwa kutetea timu
yake. Unaweza kuona kwamba huu ni mchezo mzuri kwake kwa ajili ya ujio mpya
baada ya adhabu."
0 comments