KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya
624 wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho (Septemba
14 mwaka huu).
Wachezaji wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka
watakapokamilisha taratibu ni Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon,
Godfrey Bonny Namumana (Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth
Chukwu wote wa Mwadui FC ya Shinyanga.
Darlington na Chukwu ambao wote ni Wanigeria
wamezuiwa mpaka watakapowasilisha vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara
ya Uhamiaji wakati Namumana aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati
ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Nayo African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA
Academy ambayo Namwando anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia
mchezaji huyo.
Klabu ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili
katika FDL ni Friends Rangers FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya
Shinyanga wakati iliyosajili wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu
hiyo ya Morogoro imesajili wachezaji 19 tu.
Vilevile Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili
wa wachezaji wanane wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika
hatua ya pili ya usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.
Wachezaji hao
ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na Said Ndutu
(Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal Union U20), Ramadhan
Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba) ambaye tayari Hati yake Uhamisho
wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.
0 comments