KIUNGO wa klabu ya Yanga, Mnyarwanda Haruna
Niyonzima amefichua siri iliyomsababisha akachelewa kujiunga na timu yake
iliyokuwa jijini Mbeya hivyo kukosa mchezo wao dhidi ya Mbeya City uliochezwa
mwishoni mwa wiki iliyopita.
Niyonzima ambaye ndiyo roho ya Yanga kwa sasa,
aliukosa mchezo huo baada ya kujiunga na mwenzake siku ya mchezo huo huku akiwa
mgonjwa hivyo Kocha wake, Ernie Brandts hakumtumia katika mchezo huo ambao
ulimalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani,
Niyonzima alisema kuwa kilichomsababisha kuchelewa kurudi ni matatizo ya mgongo
aliyoyapata alipokuwa akiitumikia timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ katika
mchezo wake wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani.
Niyonzima alisema alipokuwa katika kambi ya timu ya
Amavubi alishtua tatizo lake la mgongo ambalo linamsumbua kwa muda mrefu hivyo
alilazimika kubaki kwa ajili ya matibabu zaidi na alipomaliza ndipo alipoamua
kurudi.
“Haikuwa busara kuwahi kurudi wakati bado naumwa. Sasa
nimepona na nipo fiti kuitumikia klabu yangu ya Yanga kwa mafanikio zaidi,”
alisema Niyonzima.
0 comments