Meneja Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta
(kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo. Katikati ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando
na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson
Mmbando akionesha fomu za kujisajili kushiriki mbio hizo. Kulia ni Meneja Matukio wa Capital Plus,
Mathew Kasonta na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.
KAMPUNI ya Airtel ya Tanzania kupitia huduma yake ya
Airtel Money kwa mara ya tano mfululizo imetangaza kudhamini mbio za Rock City
Marathon za mwaka huu zilizopangwa kufanyika mkoani Mwanza tarehe 27, Oktoba
2013 ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya mchezo wa riadha nchini.
Airtel imekuwa mdhamini mkuu kwa upande wa
mawasiliano katika mbiyo hizo, wakishirikiana na wadhaminiwa wengine kama NSSF,
Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New
Mwanza Hotel, Sahara Communications pamoja na Umoja Switch, ili kutoa fursa ya
kuinua mchezo wa riadha inchini.
Akizungumza wakati wa tukio fupi lililofanyika
katika makao makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa
Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando alisema kampuni yake imejidhatiti
kusaidia shughuli mbali mbali za
maendeleo ya jamii na mbio za Rock City Marathon pia ni fursa pekee ya kukuza
vipaji katika michezo huo kwa ujumla.
“Kampuni ya Airtel Tanzania kwa mwaka wa tano
mfululizo, leo hii tunatangaza udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka
huu ikiwa ni sehemu ya jitihada zetu za kusaidia maendeleo ya michezo nchi
nzima.
“Tunaamini kuwa mchango wetu utasaidia katika
kuvumbua vipaji vipya vitakavyoshiriki si tu kwa mashindano ya kitaifa lakini
pia na ya kimataifa,” alisema.
Mmbando aliongeza kuwa washiriki kwa mwaka huu
wataweza kusajili moja kwa moja kupitia huduma ya kampuni yake ya Airtel Money
kwa kutuma malipo yao kwa neno MARATHON na kuhifadhi ujumbe kwa ajili ya
kuuonyesha wakati wa kuchukua fomu katika vituo mbali mbali.
Kwa upande wake mratibu wa mbio za Rock City
Marathon 2013, Bw. Mathew Kasonta wakati wa tukio alisema kuwa mbio za mwaka
huu zitakuwa kubwa na bora zaidi kwa kuleta pamoja washiriki kutoka ndani ya
nje ya nchi.
“Kwa mwaka
huu tumeungana na kampuni ya Airtel lakini kupitia Airtel Money ili kutanua
wigo wa ushiriki zaidi. Katika miaka iliyopita, watu wengi wamekuwa wakikosa
nafasi ya kushiriki au wakilazimika kusafiri umbali mkubwa kwenda kwenye vituo
vichache tulivyoviandaa ili waweze kununua fomu za usajili, kwa kupitia Airtel
Money zoezi hili litakuwa limerahisishwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Kasonta.
Kasonta aliongeza, “ukishamaliza zoezi hilo,
utapokea ujumbe utakaouonyesha pale utakapokwenda kuchukua fomu za usajili
katika ofisi za makao makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar,
Mbeya, Arusha na Mwanza.”
Alisema kuwa washiriki wenye vigezo pia wataweza
kusajili kwa kupata fomu zipatikanazo katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza,
na katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya
tatu, upande wa kulia katika jengo la ATC, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.
Kasonta alibainisha kuwa fomu za usajili
zitapatikana katika viwango vya bei vifuatavyo; shilingi 5,000 kwa mbio za km
21 (kwa watu wote), shilingi 3,000 kwa mbio za km 5 (mbio kwa makampuni na
taasisi).
Alisema kuwa fomu kwa mbio za kilometa 3 (kwa wazee
kuanzia miaka 55 na watu wenye ulemavu wa ngozi) na mbio za kilometa 2 kwa
watoto (wenye umri wa miaka 7 mpaka 10) zitapatikana bure.
0 comments