PAMOJA na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya
Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Abdallah Kibadeni amefunguka na
kusema kuwa timu yake haipo vizuri.
Kibadeni ambaye ameanza kukinoa kikosi cha Simba
msimu huu na tayari ameshacheza mechi tatu za mashindano na kufanikiwa kushinda
michezo miwili na kutoka sare mechi moja.
Simba ilifungua pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa
kucheza na Rhino Rangers ya Tabora na kuvuna pointi moja baada ya kutoka sare
ya mabao 2-2 na walikusanya pointi tatu dhidi ya JKT Oljoro kwa kushinda
bao1-0, hivyo matokeo ya jana yanawafanya wafikishe pointi saba.
Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani,
Kibadeni alisema pamoja na kupata matokeo hayo lakini kikosi chake bado
hakijakamilika kama vile anavyotaka yeye.
“Nikiwa kama kocha kuna aina ya uchezaji ambao
nautaka timu yake icheze lakini bado,” alisema Kibadeni. “Siwezi kuridhika na
ushindi ninaoupata. Kuna mambo yanataka wachezaji wangu wafanye.
“Kikosi changu bado hakijawa kamili kama ninavyotaka
na mambo hayo yakitimia Simba itakuwa tishio zaidi ya hivi inavyoonekana sasa. Tukishacheza
michezo mitano nadhani tutakuwa vizuri zaidi.”
Mchezo wa nne wa mashindano wa Kibadeni akiwa na
Simba utachezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa watakapovaana na Maafande wa
Mgambo Shooting wakati mchezo wa tano utakuwa dhidi ya Mbeya City katika uwanja
huo huo.
0 comments