Baadhi ya viongozi wapya wa Chama cha mchezo wa Ngumi
Mkoa wa Dar es salaam (DABA) wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa
uchaguzi huo, Zuwena Kipingu katikati pamoja na mwangalizi mkuu wa uchaguzi,
Remmy Ngabo (kulia) mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wao mwishoni mwa wiki
iliyopita
SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT)
halitambui uongozi uliojiingiza
madarakani wa kuongoza chama cha
ngumi mkoa wa Dar es salaam (DABA ) kiujanja ujanja bila kuzingatia Sheria na
Kanuni za Baraza la Michezo Tanzania (BMT), katiba ya Chama cha ngumi cha dunia (AIBA), Shirikisho la ngumi Tanzania (BFT) na
katiba ya Chama cha Ngumi mkoa wa Dar es salaam (DABA).
Uongozi huo ulijingiza madarakani tarehe 21/09/2013
katika ukumbi wa DDC Mlimani bila ya kuwa na kibali cha kutoka BFT wala kibali
kutoka Ofisi ya afisa michezo wa mkoa wa Dar es Salaam, ambao wao kiutaratibu
ndio walikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha kufanyika kwa uchaguzi huo na
kuusimamia kwa mujibu wa sheria zinazoongoza michezo nchini.
Badala yake genge la watu wachache walijikusanya na
kupeana fomu kinyume na taratibu kwa kujuana na hatimaye kupeana taarifa
wakakutana na kujivika madaraka kwa nyadhifa mbalimbali bila kufuata taratibu.
BFT haikubaliani na jambo hilo kwa kuwa kati ya waratibu wa zoezi hilo waliojivika uongozi wa
juu ni wale waliokuwa katika uongozi wa shirikisho la ngumi Tanzania BFT na
kupelekea Tanzania kufungiwa uanachama na chama cha ngumi cha dunia (AIBA) kwa
miaka miwili.
Pia viongozi hao ni wale waliosababisha bondia
aliyekuwa tegemeo na Taifa, Petro Mtagwa kufungwa jela miaka 15 nchini
Mauritius pia kusababisha bondia Emillian Patrick kushindwa kushiriki
Mashindano ya Olimpiki 2008 baada ya kuwa amefuzu kwa tuhuma za kula njama za
kusafirisha madawa ya kulevya.
Kibaya zaidi wengi waliopewa madaraka hawakujaza
fomu za kuomba nafasi kama walivyopewa na
hawakuwepo katika uchaguzi huo, wala hawakufanya usaili kama taratibu
zilivyo.
Wanachama halali waliokuwa wanatakiwa kuwepo katika
uchaguzi huo mfano viongozi wa chama cha ngumi Temeke hawakupewa taarifa za
uchaguzi na wameleta malalamiko ofisi za BFT.
Uchaguzi huo umekiuka katiba kwa kuhusisha mabondia
na viongozi wa ngumi za kulipwa kitu ambacho ni tofauti na katiba zote za ngumi
za ridhaa.
BFT itachukua hatua kali za kimaadili na kinidhamu
kwa wote waliohusika na zoezi hilo na kusisitiza kwa wanachama wote kuzingatia
sheria za uchaguzi wanapofanya uchaguzi wa vyama vyao na kuwataka wengine kutokujiingiza
kwa magenge ambayo historia inaonyesha wamekuwa wasubufu wa mambo mbalimbali
tokea uongozi wa Narcis Tarimo enzi za TABA kwa maslahi yao binafsi.
Zaidi tutashirikiana na Ofisi ya Afisa michezo wa
Mkoa kuhakikisha uchaguzi unafanyika wa kupata viongozi kwa kuzingatia taratibu.
0 comments