Kikosi cha Taifa Stars leo jioni kinatarajia kushuka
dimbani kuivaa timu ya Gambia katika mchezo wa mchujo wa Kombe la Dunia
utakaofanyika kwenye Uwanja wa Independence ulioko Bakau, Gambia.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
imewasili hapa jana (Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni ikitokea Dakar, Senegal
ambapo ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua kutumia usafiri wa barabara
kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko kuingia Banjul badala ya kulala na
kuchukua ndege nyingine siku inayofuata.
Wachezaji wako katika hali nzuri na jana jioni walifanya
mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Independence, Stars imefikia katika hoteli
ya Seaview iliyoko kandokando ya Bahari ya Atlantic.
Mechi ya leo inatarajia kuanza saa 10.30 jioni kwa
saa za Banjul sawa na 1.30 usiku za hapa nyumbani, na itachezeshwa na waamuzi
kutoka Rwanda Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene Ndagijimana, Honore
Simba na Issa Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka Liberia.
Washabiki na vyombo vya habari vya hapa
wanaizungumzia mechi hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia
ikiwa imeita wachezaji tisa wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo
imepata uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania
kuhakikisha haimalizi mechi za mchujo ikiwa na pointi moja tu.
Kwa upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema
nia ni kuona Stars yenye pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya
Ivory Coast ambayo tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho
kutoka kundi hili la C.
“Mechi hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka matokeo
mazuri ugenini. Lakini kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka katika
nafasi ya kuwa wa pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi kwenye
viwango vya ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi ya
sisi kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim.
Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja,
Vincent Barnabas, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo,
Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha.
0 comments