Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
amesema wanaipa umuhimu mkubwa mechi ya mwisho ya mchujo ya Kombe la Dunia
dhidi ya Gambia kwa lengo ni kuhakikisha wanamaliza wakiwa wa pili katika kundi
hilo.
Mechi hiyo itachezwa Septemba 7 mwaka
huu jijini Banjul, Gambia ambapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premiem Lager itaondoka kesho (Septemba 4 mwaka huu) saa 11 alfajiri kwa ndege
ya Kenya Airways kupitia Dakar, Senegal.
Kim amesema wanataka kushinda ugenini,
kwani licha ya kuwa wameshatolewa lakini ushindi utawaongezea pointi kwa ajili
ya viwango (rankings) vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na
pia kuepuka kuanzia ngazi ya awali ya mechi za mchujo za Kombe la Mataifa ya
Afrika (AFCON) kwa fainali za 2015.
“Tunacheza mechi hii tukiwa katika mazingira
magumu, kwani wengi wa wachezaji wa kikosi cha kwanza ni majeruhi. Sijawahi
kukutana na hali hii tangu nilipoanza kuifundisha Taifa Stars, lakini
tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Kim.
Amesema kwa mipango ya timu yake mechi
hiyo ni muhimu tofauti na wengi wanavyofikiria, na uamuzi wake wa kumwita beki
Henry Joseph amezingatia mambo mengi ya kiufundi ikiwemo nafasi anayocheza na
uzoefu wa mchezaji aliyekuwa akicheza nchini Norway katika klabu ya Kongsvinger
IL.
Wachezaji majeruhi katika kikosi hicho
ni Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Athuman Idd
na John Bocco.
Vilevile wachezaji Mbwana Samata na
Thomas Ulimwengu hawatakuwemo kwenye safari baada ya klabu yao ya TP Mazembe
kutuma taarifa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo mchana ikidai ni
wagonjwa.
Wachezaji wanaoondoka kwenda Banjul ni
Juma Kaseja, Mwadini Ali, Ali Mustafa, Amri Kiemba, David Luhende, David
Mwantika, Erasto Nyoni, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Henry Joseph, Jonas
Mkude, Juma Liuzio, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Said Dilunga,
Simon Msuva na Vincent Barnabas.
0 comments