KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema uwakilishi wa ujumbe kwenye Mkutano
Mkuu unaanzia kwenye chama cha mpira wa miguu cha mkoa, kufuatiwa na chama
shiriki na baadaye klabu ya Ligi Kuu.
Mwongozo huo juu ya uwakilishi wa wajumbe kwenye
Mkutano Mkuu umetolewa kutokana na maombi ya Sekretarieti ya TFF kwa kamati
hiyo iliyokutana jana (Septemba 16 mwaka huu) baada ya kubaini baadhi ya
wajumbe wanashikilia nafasi mbili kwenye vyama tofauti.
Kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba, kuna makundi ya
aina tatu ya wanachama wanaounda TFF. Makundi hayo ni vyama vya mikoa, vyama
shiriki na klabu za Ligi Kuu.
Sekretarieti ya TFF imebaini kuwa kuna baadhi ya
viongozi wa kuchaguliwa wa mikoa ambao pia ni viongozi wa vyama shiriki na
klabu za Ligi Kuu, hivyo wana nafasi zaidi ya moja ya kuingia kwenye Mkutano
Mkuu.
Hivyo, kutokana na mwongozo huo ushiriki wa wajumbe
kwenye Mkutano Mkuu wa TFF utaanzia chama cha mkoa, kufuatiwa na chama shiriki
na baadaye klabu za Ligi Kuu.
Pia nafasi ambazo zinaweza kuwakilishwa kwenye
Mkutano Mkuu kama mhusika hayupo ni za Mwenyekiti atakayewakilishwa na Makamu
Mwenyekiti, na Katibu atakayewakilishwa na Katibu Msaidizi. Nafasi za ujumbe wa
Mkutano Mkuu na ile ya mwakilishi wa klabu hazina uwakilishi kama mhusika
hayupo.
0 comments