KUNDI la muziki wa kizazi kipya la East Coast Team ‘ECT’
lenye maskani yake Upanga Mashariki, ambalo hivi karibuni limerudi tena kwenye
tasnia hiyo na tayari wameanza kutupa mawe kwa mahasimu wao wakubwa TMK
Wanaume.
ECT ambalo lilipata umaarufu mkubwa mwanzoni mwa
miaka ya 2000 lakini lilivunjika baada ya wasanii wake mahiri kuanza kufanya
kazi zao binafsi wakati TMK Wanaume waligawanyika na kuzaliwa makundi mawili
TKM Wanaume Halisi na TMK Wanaume Family.
Kundi la ECT linaloongozwa na Gwamaka Kaihula
anayejulikana zaidi kama King Crazy GK limeundwa upya likiwa na wasanii
walewale na wengine wapya na tayari wameanza kutambulisha ujio wao mpya kwa
kuachia wimbo mpya wa kiongozi wa kundi hilo GK uliopewa jina la ‘Baraka au Laana kuzaliwa Afrika’.
Wasanii wanaounda kundi hilo kwa sasa ni GK, Ambwene
Yessaya ‘AY’, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, Adam Semkwiji ‘Snare’, Benjamin Gemba
‘Buff G’, Juma Mtanga, Sheila ‘Lady Slay’, Sharrif na Yussuph Seleman ‘Yuzo’ na
wengine wanatarajia kuongezeka baada ya kufanyika mchujo wa wasanii wenye uwezo
wa kuingia katika kundi hilo.
GK alipokuwa akizungumza na Nyumba ya Michezo ya Burudani
alisema kwa sasa wamerudi kwa kishindo na wamekuja kivingine kabisa na kiukweli
hawawezi kushindana na TMK Wanaume kwani kwa sasa hawawezi kuwaita washindani
wao kwa kuwa hawawezi kufikia viwango vyao walivyokuja navyo sasa.
“Inakuwa ngumu kusema tumerudi kushindana na TMK
kwani wakati wapo pamoja walikuwa hawatuwezi sasa wametengana ndiyo kabisa
hawawezi kuufikia muziki wetu,” anasema GK. “Labda warudi waungane upya na
wafanye muziki kwa viwango vya kimataifa ndipo wataweza kushindana na sisi.”
GK alisema anaomba kundi la TMK lirudi na wafanya
muziki kwa kiwango chao ili waweze kuwa na ushindani kwani bila ushindani
muziki hauwezi kuendelea lakini pia hamasa ya muziki utakuwa chini kwa kuwa
hakuna kitu ambacho kinawafanya wasanii wafanye kazi kwa bidii.
GK alisema: “Enzi zile kulikuwa na watu wanatembea
kwa miguu kutoka Temeke hadi Diamond kuja kuangalia show ya ECT na Wanaume.
Show ambazo ECT na Wanaume walikuwepo zilikuwa zinafanya vizuri sana kutokana
na ushindani wa makundi haya.”
0 comments