LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu
kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio
ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na
ile kati ya Mbeya City na Yanga.
Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana
kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na
kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A
itakuwa sh. 20,000.
Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya
mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo
haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.
Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya,
shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC.
Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna
wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.
Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na
Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting
(Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja
wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex, Dar
es Salaam).
0 comments