PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji
Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000.
Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo
namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi
wa mabao 3-2 walikuwa 24,020.
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh.
8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
21,079,525.42.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya
uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh.
10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa
Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) sh. 3,923,014.64.
Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya
Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000.
Pia taarifa nyingine TFF imesema kuwa mechi namba 12
ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Toto Africans na Polisi Dodoma iliyokuwa
ichezwe Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo za kundi C sasa zitapambana Jumapili
(Septemba 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo ili kupisha mechi namba 10 kati
ya Pamba na Stand United FC ya Shinyanga itakayochezwa Jumamosi (Septemba 28
mwaka huu).
Mechi nyingine za kundi hilo zitakazochezwa Jumamosi
ni Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) wakati Kanembwa JKT
na Polisi Mara zitacheza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
0 comments