Uongozi wa klabu ya Yanga umewapiga chenga ya mwili
wazee wa klabu hiyo baada ya kukanusha kufanyika kwa mabadiliko yaliyofanyika
kuondolewa kwa katibu wake, Lawrence Mwalusako na nafasi yake kuchukuliwa na
Mkenya.
Wazee wa Yanga walitoa tamko lao juzi kuupa uongozi
huo masaa 24 kumtimua kati huyo mpya, Patrick Naggi hali iliyosababisha uongozi
huo kukutana na kujadili suala hilo.
Akizungumza Nyumba ya Michezo na Burudani, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement
Sanga alisema taarifa za kuondolewa Mwalusako na kuajiriwa Mkenya hazina ukweli
kwamba tayari kuna mtu amechukua nafasi yake, kilichotokea ni kutokuwepo kwa
mawasiliano mazuri katika suala hilo kati ya viongozi na wazee.
Sanga alisema kilichopo ni kwamba uongozi wa klabu
ya Yanga upo katika mchakato wa kuhakikisha unajaza nafasi zilizopo wazi za
mkurugenzi wa ufundi, mkurugenzi wa masoko, mkurugenzi wa fedha na zoezi hilo
linaendeshwa na kampuni moja ambayo waliipa nafasi ya kuendesha zoezi hilo.
Zoezi likiwa ndani ya mchakato mmoja wa waombaji wa
nafasi hizo Patrick Naggi aliwasili makao makuu ya klabu ya Yanga kwa lengo la
kutaka kujua mazingira ya ufanyaji kazi yakoje na kufahamu baadhi ya mambo
kuhusiana na klabu ndipo kulipotokea kutokuelewana na baadi ya wanachama
wakiwemo wazee waliokuwepo eneo la klabu.
Makamu huyo alisema anapenda kutoa taarifa kwa umma
na wanachama wa Yanga kuwa uongozi bado haujatoa baraka za ajira kwa mtu yoyote
katika nafasi hizo, isipokuwa ni muombaji aliwahi kufika makao makuu kabla ya
mchakatao wa usahili kukamilika.
Alisema Mwalusako anaendelea kuwa kaimu katibu mkuu
wa Yanga mpaka hapo kutakapokuwa na taarifa nyingine zozote za mabadiliko kwa
nafasi zote zilizopo wazi katika idara mbalimbali.
Uongozi unawaaomba wanachama, wapenzi na washabiki
wa soka kuwa kitu kimoja katika kuunga mkono harakati za kimaendeleo ili
kuifanya timu iende katika hatua nyingine ya ushindani wa kimatifa.
0 comments