TAIFA Stars sasa inacheza na Zimbabwe mechi ya
Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)- FIFA Date
itakayofanyika keshokutwa Jumanne (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Awali Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager ilikuwa icheze na Kenya (Harambee Stars), lakini Shirikisho la
Mpira wa Miguu Kenya (FKF) lilituma taarifa jana jioni (Novemba 16 mwaka huu)
likieleza kuwa timu yake haitacheza tena mechi hiyo.
Kikosi cha Zimbabwe chenye msafara wa watu 30
kinatarajia kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
kesho (saa 3 asubuhi) tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11 kamili
jioni.
Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Uganda wakati
Kamishna atakuwa Leslie Liunda wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa mezani ni Oden
Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Stars chini ya Kocha Kim Poulsen ipo kambini tangu
Novemba 12 mwaka huu kujiwinda kwa mechi hiyo. Kim amejumuisha kwenye kikosi
chake wachezaji watano wanaocheza mpira wa miguu nje ya Tanzania.
Kiingilio katika mechi ya kirafiki ya kimataifa kati
ya wenyeji Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe ni sh. 5,000 wakati tiketi
zitaanza kuuzwa Jumatatu (Novemba 18 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini
Dar es Salaam.
Mbali ya kiingilio hicho cha sh. 5,000 ambacho ni
kwa viti vya bluu na kijani, viingilio vingine ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh.
20,000 kwa VIP B, sh. 15,000 kwa VIP C wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh.
10,000.
Tiketi zitauzwa katika magari maalumu katika vituo
vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio
na Samora, Sokoni Kariakoo, Dar Live Mbagala, OilCom Ubungo, BMM Salon iliyopo
Sinza Madukani, Uwanja wa Uhuru, mgahawa wa Brake Point uliopo Kijitonyama, na
kituo cha mafuta Buguruni.
0 comments