KOCHA wa zamani wa Azam, Stewart Hall amesaini
mkataba wa kufundisha chuo kipya cha Sunderland cha Kidongo Chekundu kwa lengo
la kuibua na kukuza vipaji vya wachezaji nchini.
Akizungumzia jana baada ya kusaini mkataba huo, Hall
alisema amefurahi kupata nafasi hii hapa Tanzania katika mpango huu wa
kuendeleza vipaji vya wachezaji vijana katika klabu zote na timu ya taifa.
“Chipukizi watakuwa wakifundishwa mbinu, ufundi,
nguvu na kuwaandaa kwa ajili ya kucheza soka ya kisasa. Pia kutakuwa na mafunzo ya ukocha.”
Hall aliongeza, “Wachezaji watakaokuwa bora zaidi
watakuwa wakipata nafasi ya kufanya majaribio katika akademi ya Sunderland ya
Light Uingereza.”
Mtendaji Mkuu wa Symbion Power Tanzania, Peter
Gathercole alisema Hall atakuwa meneja wa kijiji cha michezo cha Kidongo
Chekundu Sports Park na Elite Football Academy.
Gathercole alisema ujenzi wa kituo hicho utakaoanza
mwezi huu utakuwa na viwanja vya kisasa 3G vyenye nyasi bandia na viwanja
vitano vidogo kulingana na umri. Pia
kutakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya matibabu na sehemu ya
chakula.
Naye Mkurugenzi wa Sunderland AFC, Margaret Byrne,
alisema: “Tungependa kuona akademi hii inakamilika kwa wakati. Tumemchagua
Stewart kuendeleza chuo hiki ni matumaini yetu kila mmoja atajitoa katika
kuhakikisha tunapata matunda yake katika siku za karibuni.”
Hall, ambaye ni kocha mwenye leseni ya UEFA na
mkufunzi wa UEFA, hivi karibuni alivunja mkataba wake na klabu ya Azam.
Pia, aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Zanzibar,
alikuwa Mkurugenzi wa akademi ya Birmingham City. Mbali na hiyo Hall aliwahi kuwa kocha timu ya
taifa ya Saint Vincent na Grenadines na timu ya Pune FC ya India.
0 comments