Na Erasto Stanslaus
SIMBA ya Dar es Salaam
imeanza kufuata nyayo za msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Bara zilizoifanya ianze
vizuri lakini ikaishia kushika nafasi ya tatu.
Klabu hiyo ilianza
msimu ikiwa na kocha Milovan Cirkovic lakini katikati ya msimu ikamtimua na
nafasi yake ikachukuliwa na Mfaransa, Patrick Liewig aliyetimuliwa mwishoni mwa
msimu.
Msimu huu, Simba
ilianza kunolewa na Abdallah Kibaden akisaidiwa na Jamhuri Kihwelu ambao
wametupiwa virago. Taarifa zinasema kwamba ataajiriwa Zdravko Logarusic wa
Croatia aliyewahi kuifundisha Gor Mahia ya Kenya.
Katikati ya msimu
uliopita Simba, uliibuka mgogoro wa uongozi ambao ulipelekea baadhi ya wajumbe
wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu. Msimu huu Kamati ya Utendaji imemsimamisha
Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.
Sababu za kusimamishwa
kwake ni danadana kuhusiana na ziliko fedha za uuzwaji wa mchezaji wao Emmanuel
Okwi pamoja na kutojishughulisha sana na masuala ya klabu. Okwi aliuzwa katika
klabu ya Étoile du Sahel ya Tunisia kwa dola 300 (Sh. 480 milioni).
Rage ndiye alifanya
mazungumzo na Étoile na ndiye aliyekamilisha dili la kumuuza lakini fedha hizo
hazikufika klabuni. Fedha hizo ndiyo sababu ya kukorofishana na tawi la Mpira
Pesa.
MAKALA IMETOKA GAZETI
LA MAWIO
0 comments