KOCHA Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni leo ameshusha
presha ya kutaka kung’olewa katika klabu hiyo baada ya kuibuna na ushindi wa
mabao 4-2 dhidi ya Ashanti United uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikitoka kutoa sare tatu dhidi ya Yanga (3-3),
Coastal Union (0-0) na Kagera Sugar (1-1) na kufungwa 2-1 na Azam, Simba SC leo
ilipata ushindi wake kupitia kwa Betram Mombeki aliyefunga mawili, Amisi Tambwe
na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Pamoja na ushindi huo, Simba SC inabaki nafasi ya
nne kwa pointi zake 24, baada ya kucheza mechi zote 13 za mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu. Azam na Mbeya City zina pointi 26 kila moja na Yanga inafuatia kwa
pointi zake 25 na timu zote hizo zitacheza mechi zake za mwisho kesho.
Simba SC walitangulia kupata bao dakika ya nane
kupitia kwa winga wake machachari, Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyepasua
katikati ya ukuta wa Ashanti baada ya pasi ya Amisi Tambwe kabla ya kumchambua
kipa mkongwe, Amani Simba.
Ashanti walisawazisha dakika ya 45 mfungaji, Hussein
Swedi aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Hussein Mkongo kutoka wingi
ya kulia.
Timu hizo zilishambuliana kwa zamu kipindi cha
kwanza, Ashanti wakigonga pasi fupi fupi zenye kusisimua na Simba wakitumia
mipira mirefu kushambulia kupitia kwa washambuliaji wake wawili, Tambwe na
Betram Mombeki.
Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na Kocha
mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kuwatoa wakongwe Henry
Joseph na Amri Kiemba na kuwaingiza chipukizi Said Ndemla na William Lucian
‘Gallas’ yaliisaidia Simba kupata ushindi.
Amisi Tambwe alifunga bao la pili dakika ya 46 tu
akipokea pasi ya Singano ‘Messi’ na Mombeki akafunga la tatu dakika ya 50,
akiunganisha krosi ya Haruna Shamte.
Mkongwe Said Maulid ‘SMG’ aliifungia Ashanti bao la
pili dakika ya 53 kwa pasi ya Hussein Swedi, lakini Mombeki akaihakikishia
Simba SC ushindi kwa bao zuri dakika ya 61 akiunganisha krosi ya Shamte tena.
Simba SC ingepeta mabao zaidi kama ingeweza kutumia
nafasi zaidi ya mbili nzuri ilizotengeneza. Kipa Amani Simba alitolewa nje kwa
kadi nyekundu dakika ya 90 baada ya kudakia nje ya eneo lake mpira. Nahodha Paul Maona alimpisha kipa Daudi Mwasongwe
akamalizie mchezo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abuu Hashimu, Haruna
Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze, Hassan Hatibu/Hassan Isihaka
dk75, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Henry Joseph/Said Ndemla dk46,
Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Amri Kiemba/William Lucian dk46.
Ashanti United; Amani Simba, Hussein Mkongo, Jaffar
Gonga, Tumba Swedi, Samir Ruhava, Iddi Said, Fakih Hakika, Paul Maona/Daudi
Mwasongwe dk90, Hussein Swedi, Said Maulid ‘SMG’/Abdul Kimbirwa dk83 na Joseph Mahundi.
0 comments