TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo
imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kulazimishwa suluhu na
Zimbabwe jioni hii katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Hata hivyo, Zimbabwe wangeondoka na sherehe Uwanja
wa Taifa, kama si Refa Ronnie Kalema aliyesaidiwa na Samuel Kayondo na Lee
Okelo wote kutoka Uganda kuwakatalia bao zuri lililofungwa na Sithole Simba
dakika ya 90.
Kwa ujumla, Tanzania haikuwafurahisha mashabiki wake
leo pamoja na kuwa na kikosi chake kamili, wakiwemo washambuliaji tegemeo
Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe ya DRC, kiungo Mwinyi
Kazimoto anayechezea Al Markhiya ya Qatar na beki Shomari Kapombe anayechezea
AS Cannesd ya Ufaransa.
Stars iliuanza vyema mchezo huo, safu ya kiungo
ikiundwa na chipukizi Hassan Dilunga aliyecheza pamoja na Frank Domayo na
Mwinyi Kazimoto.
Viungo hao waliweza kuwachezesha vizuri
washambuliaji watatu wa Stars, Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu na Mbwana
Samatta, lakini wakashindwa kutumia nafasi hizo vizuri kipindi cha kwanza.
Zimbabwe walizinduka baada ya dakika 10 na kucheza
vizuri, wakitengeneza nafasi pia ambazo walishindwa kuzitumia.
Safu ya kiungo ya Stars ilikufa ndani ya dakika 30
na Zimbabwe wakaanza kutawala mchezo. Kipindi cha pili, Kim alifanya mabadiliko
ya viungo akiwaingiza Amri Kiemba na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuchukua nafasi
za Kazimoto na Dilunga na kidogo Stars ilianza kutawala sehemu ya katikati ya
Uwanja, lakini iliishia kukosa mabao ya wazi.
Nafasi ambayo Stars wataijutia zaidi ni ya dakika ya
75, kufuatia Kapombe kutia krosi nzuri baada tya kupokea pasi ya Sure Boy, lakini
Ulimwengu akazidiwa na kipa Tapiwa Kapini aliyedaka mpira miguuni mwake.
Kipa Ivo Mapunda alifanya kazi nzuri kwa kuokoa
michomo mitatu ya hatari hali ambayo ilifanya ashangiliwe baada ya mechi.
Mashabiki walimzomea kocha Mdenmark Kim Poulsen
baada ya mechi wakimuambia timu imemshinda na kumtaka aondoke.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ivo Mapunda, Shomari
Kapombe, Erasto Nyoni/Himid Mao dk56, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Frank
Domayo, Hassan Dilunga/Salum Abubakar dk51, Mwinyi Kazimoto/Amri Kiemba dk51,
Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa/Farid Mussa dk80.
0 comments