Na
Erasto Stanslaus
KIM Poulsen, Kocha mkuu
wa Taifa Stars aliyejijengea umaarufu kwa kutengeneza kikosi kamambe cha
ushindi, sasa anasumbuliwa na Matokeo Makubwa Sasa.
Mipango yake ni ya
dharura. Kocha huyo aliyekuwa anategemea timu za vijana za Ngorongoro Heroes
(U-20) na Serengeti Boys (U-17) kama vitalu vya kupata wachezaji wa baadaye wa
Stars amebadilika ghafla na kubaki akitegemea wakongwe.
Mfano, katika uteuzi wa
Stars hivi karibuni Kim aliamua kutengeneza kundi jipya lisilo na daraja
akaliita Future Young Stars yaani Nyota wa Stars ya Baadaye.
Kundi hilo la Future
Young Stars ni la akina Aishi Manula, Hussein Shariff, Ivo Mapunda, David
Luhende, Hassan Mwasapili, Himid Mao, Issa Rashid, Ismail Gambo, John Kabanda,
Kessy Khamis, Michael Pius, Miraji Adam, Mohamed Hussein, Said Moradi na Waziri
Salum.
Wengine ni Amri Kiemba,
Farid Mussa, Haruni Chanongo, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Khamis Mcha,
Ramadhan Singano, Simon Msuva, William Lucian, Elias Maguli, Hussein Javu,
Joseph Kimwaga, Juma Liuzio, Mwagane Yeya na Paul Nonga.
Lakini aliowaita kuunda
Taifa Stars ni Ally Mustafa, Mwadini Ali, Aggrey Morris, Kelvin Yondani,
Shomari Kapombe, Nadir Haroub, Erasto Nyoni, Vincent Barnabas, Salum Abubakar,
Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Athuman Idd, Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu,
Mbwana Samata na John Bocco.
Wachezaji 16 kutoka
Future Young Taifa Stars wameungana na 16 wa Taifa Stars kuunda timu kamili
ambayo ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe na kutoka suluhu. Stars
ilielemewa sana hasa kipindi cha pili na mashabiki wa Stars hawakuridhishwa na
kiwango cha kikosi hicho hivyo walipandwa na hasira na kuanza kumzomea Kim mara
baada ya mchezo kumalizika.
Tujiulize, Ivo Mapunda
aliyeichezea Stars akaachwa kwa madai kiwango kimeshuka nafasi yake ikatwaliwa
na Juma Kaseja bado leo tunaambiwa ni Future Young Taifa Stars?
Umri wa Amri Kiemba
ambaye leo anaitwa matumaini ya baadaye ni mkubwa kuliko Frank Domayo au
Aboubakar Salum ambao ni matumaini ya sasa. Nani alipaswa kuwa matumaini
ya baadaye kati ya wachezaji hao?
Inawezekanaje Said
Morad na Hussein Javu wawe matumaini ya baadaye wakati Thomas Ulimwengu na
Shomari Kapombe ni mategemeo ya sasa?
Hapa ni wazi kuwa Kim
ama amefikia ukomo wa ujuzi wake au anataka Matokeo Makubwa Sasa. Anataka timu
ya kushinda michezo sasa na siyo hicho kiitwacho Future Young Taifa Stars.
Kwa mfumo anaoutumia
Kim kuwategemea vijeba zaidi kuliko vijana ni ngumu kupata mafanikio yenye
mwendelezo. Inawezekana timu ikaonekana ‘bora’ sasa lakini ikapotea kabisa
katika ramani ya soka.
Kama kweli Kim angekuwa
na nia ya kweli ya kuiboresha Stars baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza
fainali za Kombe la Dunia mwakani na zile za Afrika, ulikuwa muda muafaka wa
kutengeneza kikosi cha baadaye cha Stars kwa kuwatumia wachezaji vijana wa
Serengeti na Ngorongoro.
Hii inaonesha kuwa
hakuna mipango ya kufanya vizuri kwa miaka ya baadaye kwani mfumo huu
unawapoteza wachezaji vijana na kuwabeba vijeba ambao safari yao kisoka
imefikia tamati.
MAKALA IMETOKA GAZETI
LA MAWIO
0 comments