KOCHA Mkuu wa klabu ya Azam FC, Stewart John Hall
ameitosa kwa mara nyingine timu hiyo muda mchache baada ya kumalizika kwa
mchezo wao dhidi ya Mbeya City ambao uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Kocha huyo raia wa Uingereza mara baada ya
kumalizika kwa mchezo huo aliwaaga wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi baada
ya kukubaliana na uongozi wa klabu hiyo.
Hall kuiacha Azam ni mara ya pili kwani mara ya
kwanza aliondoka katika kikosi hicho Agosti mwaka jana lakini alirudi tena
baada ya timu hiyo kumtaka kocha huyo alejee tena kuinoa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo
kupitia tovuti yake, imedai kuwa wameachana na Hall ambaye ameomba kufanya
hivyo kwani anataka kupata changamoto mpya kutoka katika klabu nyingine.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa pande zote mbili
zimekubalina kuvunja mkataba huo baada ya mazungumzo marefu na uongozi
unamtakia kila la kheri huko aendako na unamshukuru kwa mafanikio aliyoipatia
timu hiyo.
Hall anaiacha Azam ikiwa katika nafasi ya pili
katika msimamo wa ligi hiyo baada kujikusanyia pointi 27 huku ikiwa na rekodi
ya kutopoteza mchezo katika mzunguko wa kwanza.
Muingereza huyo aliondoka baada ya kuiwezesha Azam
kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Kombe la Kagame, pamoja na kuiwezesha
kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.
Hata hivyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia
kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.
Stewart akarudia kuipa nafasi ya pili Azam katika
Ligi Kuu na kuipa Kombe la Mapinduzi pamoja na kuiwezesha kutwaa taji la Ngao
ya Hisani, michuano iliyofanyika mjini Kinshasa, DRC, Desemba mwaka jana.
Bado haijajulikana sasa Azam itaangukia mikononi mwa
kocha gani, ikiwa sasa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika na wachezaji
wanakwenda mapumzikoni.
Stewart ni kocha wanne kuondolewa Azam tangu ianze
kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007/2008 baada ya Wabrazil Neider dos Santos na
Itamar Amorin na Mserbia Bunjak.
0 comments