NYASI za uwanja wa shule ya msingi Ubungo jijini Dar
es Salaam leo zinatarajiwa kuwaka moto wakati timu ya wanamuziki wa bendi ya
Extra Bongo na kundi la Sanaa ya Maigizo la Jakaya watakaposhuka dimbani
kumenyana katika mechi ya kirafiki maalumu kwa ajili ya kuzindua 'Extra Bongo
Funs'.
Kwa mujibu wa msemaji wa bendi hiyo Juma Kasesa,
maandalizi ya mchezo huo yamekamilika ambapo kwa wiki kadhaa sasa vikosi vya
timu zote vimekuwa kwenye mazoezi makali kujiwinda na mchezo unaovuta hisia za
mashabiki wa soka waliokamia kumuona Mkurugenzi wa Extra Bongo Kamarade Ally
Choki akicheza beki wa kati (mkoba).
Alisema, mechi hiyo ni muendelezo wa bendi hiyo
kuongeza wigo mpana wa marafiki kwa ajili ya kujiimarisha katika ushindani wa
muziki wa dansi lengo lengo likiwa ni kuwafikia popote walipo.
Alieleza, mchezo huo licha ya kudumisha urafiki wao
pia utasaidia kuimarisha afya ya miili ya wachezaji wa pande zote mbili ili
kukabiliana na magonjwa nyemelezi na mara baada ya mechi hiyo wameshaomba
kukipiga na kundi lingine la sanaa Bongo Movie.
Aliwataja baadhi ya nyota wa bendi hiyo watakaoshuka
dimbani wakiongozwa na nahodha wao Salum Chakuku 'Chakuku Tumba' kuwa ni
Athanas Muntanabe, Super Nyamwela, Redo Mauzo, Efraim Joshua, Adam Hassan,
Hosea besi, Danger Boy, Adam Bombole na Ally Koncho ambao wameapa kuadhibu
wapinzani kutokana tambo nyingi ambazo wamekuwa wakizitoa dhidi yao.
Kwa upande Mkurugenzi wa Jakaya Arts linalorusha
mchezo wake katika kituo cha runinga cha ITV kila Jumamosi, Devid Mponji,
alisema, wamejiandaa vya kutosha kuikabili Extra Bongo na kwa kiwango cha safu
yake ya ushambuliaji Choki atakuwa uchochoro wa kuruhusu kufungwa mabao mepesi
kwakuwa hatoweza kumudu kasi waliyonayo.
Alisema,kikosi chake kinanolewa na kocha wa timu ya
Kijogoo maarufu kwa jina 'Kikoti' chini
ya nyota wake Erick Mikongoti, Rashidi Mawala, Omary Zero na nahodha Jose
Mawala.
0 comments