WACHEZAJI watano wa timu ya Yanga wameongeza
mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani
yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa
mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya
kuitumikia klabu ya Yanga ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub
"Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ (2014-2016),
mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016).
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Yanga,
Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza
taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka
mwaka 2016.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji
wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao
tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda
mrefu "alisema Bin Kleb.
Wakati huo huo kikosi cha Yanga leo kimeanza mazoezi
asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa
hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
0 comments