MWENYEKITI wa Simba, Ismail Aden Rage ameagizwa
kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia sasa.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa
agizo hilo baada ya kubaini kuwa mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua
mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na
nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.
Kwa maagizo hayo kutoka TFF kwenda kwa Rage ina maanisha kuwa shirikisho hilo limetambua nafasi yake kama mwenyekiti na kutupilia mbali barua ya Kamati ya Utendaji ya Simba iliyomsimamisha.
TFF kama ingetambua barua ya Kamati ya Utendaji ya Simba basi angepewa maagizo Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi' kuitisha mkutano huo badala ya Rage aliyesimamishwa.
Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6)
ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF,
itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha
kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”
TFF itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na
kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata
fursa ya kusikilizwa.
0 comments