MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara
unatarajia kumalizika kwa michezo ya kesho Novemba 6 na keshokutwa Novemba 7
huku kukiwa na sintofahamu nani atamaliza akiwa kileleni.
Imekuwa na mazoea kuwa katika ligi hiyo timu
zinazokuwa kileleni ni Yanga, Azam na Simba SC lakini msimu huu ni tofauti
kutokana na ushindani ulioibuka kutoka kwa timu kama Mbeya City.
Mbeya City, timu ambayo ni mpya katika ligi hiyo imeongeza
ushindani mkubwa na kuna uwezekano ikamaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika
kileleni mwa msimamo.
Timu hiyo inayonolewa na Juma Mwambusi ipo katika
nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 26 sawa na vinara Azam
FC na timu hizo zitamaliza mzunguko huo kwa kuvaana mechi ambayo itatoa maamuzi
nani atakuwa kinara.
Michezo ya mwisho itakuwa kama ifuatavyo, Novemba 6
ni JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Ashanti United na Simba Uwanja
wa Taifa, Kagera Sugar na Mgambo Shooting Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na Ruvu Shooting
dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini.
Novemba 7 kutakuwa na mechi kati ya Azam FC na Mbeya
City Chamazi, Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Rhino
itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora.
Mechi ambazo zinatarajiwa kuteka hisia za mashabiki
wa soka nchini ni zitakazochezwa Novemba 7 kati ya Yanga na Oljoro, lakini kwa
maana ya mechi ya kufungia msimu, basi itakuwa Chamazi Azam na Mbeya City.
Mshindi wa mechi hiyo moja kwa moja atamaliza
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu akiwa kileleni, na atakayefungwa anaweza
kuporomoka hadi nafasi ya tatu, iwapo Yanga SC itashinda mechi yake na Ojoro.
Wakitoka sare, Azam itabaki juu ya Mbeya City na Yanga inaweza kupanda kileleni
ikishinda.
Mbeya City na Azam ndizo timu pekee ambazo hadi sasa
msimu huu hazijapoteza mechi, wakati mabingwa watetezi, Yanga waliopoteza mechi
moja tu mbele ya Azam, wanakaa nafasi ya tatu kwa pointi zao 25.
0 comments