Msanii Judith Wambura ‘Lady Jaydee akipagawisha kwenye
tamasha la Kili Music Tour lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mbeya City Mjini
Mbeya.
TAMASHA la wasanii
la Kili Music Tour juzi (Jumamosi) llifanyika kwenye Ukumbi wa New Mbeya City
Club, ambapo wasanii mbalimbali walitoa burudani ya aina yake.
Katika tamasha
hilo ambalo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia bia yake ya
Kilimanjaro, wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya na Hip Hop walitoa
burudani kali na kuwaacha mashabiki midomo wazi kutokana na kufanya kile
ambacho hawakutegemea.
Katika tamasha hilo,
ambalo lilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa muziki kutoka katika Mkoa wa
Mbeya na maeneo ya karibu, lilianza jioni ambapo msanii mwenyeji Awilo wa Mbeya
alianza kwa kuimba baadhi ya nyimbo ikiwa ni pamoja na zile za asili.
Baada ya msanii
huyo, alipanda jukwaani Snura na kuimba baadhi ya vibao vyake ikiwa ni pamoja
na Nimevurugwa na Majanga ambavyo viliwafanya mashabiki walipuke kwa
kumshangilia kwa kiasi kikubwa.
Baadaye alipanda
Linex ambaye alionekana kukonga nyoyo za mashabiki wake kutokana na staili
tofauti aliyoingilia na kushuka chini ya jukwaa ambapo aliimba sambamba na
mashabiki wake.
Barnaba Elius
alipanda baada ya kushuka kwa Linex, na kuimba baadhi ya nyimbo na baadaye
alifuatia Ben Paul na kuimba nyimbo kadhaa ikiwa ni pamoja na wimbo wake mpya
wa Wa Ubani aliomshirikisha Alice.
Kwenye tamasha
hilo ambalo limebeba ujumbe wa Kikwetu kwetu,
lilimfanya Kala Jeremiah aliyejizolea tuzo nyingi za Kilimanjaro Music
Awards, kuamsha hisia za watu kutokana na kuimba nyimbo kama vile Dear God, Ningekuwa
Rais na Wimbo wa Taifa.
Izzo Business
ambaye ndio alikuwa msanii mwenyeji kwenye tamasha hilo aliwafanya mashabiki
wake wamshangilie kwa staili ya tofauti kutokana na kuimba nyimbo kama vile
Ongea na Mshua, Nakuchukia Mwaka jana na Love Me aliyemshirikisha Barnaba
Elius.
Wasanii wa Hip Hop
Farid Kubanda ‘Fid Q’ na Joseph Haule waliwafanya mashabiki kuwa na hisia kali
kutokana na tng zao kiasi ya kwamba Polisi waliokuwa wakiangalia usalama
kufanya kazi ya ziada na kuwalazimisha kushuka jukwaani kabla ya kupanda kwa
Judith Wambura ‘Lady Jaydee na baadaye Profesa Jay alipomalizia onyesho hilo
kwa kuimba baadhi ya nyimbo ikiwa ni pamoja na zile za zamani kama vile
Niamini, Piga Makofi, Hapo Vipi na Kamili Gado.
0 comments