Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Maalim 'Gurumo'
MWANAMUZIKI mkongwe wa kundi la Msondo Ngoma,
Muhidin Mwalimu 'Gurumo', ametangaza rasmi kustaafu shughuli za muziki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Gurumo, alisema
ameamua kustaafu muziki kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa na kushindwa
kumiliki vizuri changamoto za kazi hiyo.
Gurumo alisema amekuja kuwaaga rasmi mashabiki wake
kuwa muziki hataki kuendelea nao tena na ameona apumzike na kuendelea na
majukumu ya kulea familia yake vizuri.
"Tangu nimeanza muziki 1954 hadi sasa sijapata
hata baiskeli katika kazi yangu hii, hivyo nimeona suala la msingi ni kuuacha
nikiwa na umri huu.
"Licha ya kustaafu muziki, sitawatenga wasanii
pamoja na kundi langu, nitaendea kuwa pamoja nao na nitaendelea kuwa mshauri
wao pale nitakapohitajika kufanya hivyo," alisema Gurumo.
Aliongeza kuwa ameteuwa kamati kwa ajili ya
kumsaidia mambo yake mengine ikiwa ni pamoja na harakati za kuwaaga mashabiki
wake kisanii.
''Tumeanda tamasha kwa kushirikiana na kamati
niliyoiteua, ambalo nitapanda jukwani kuimba kwa mara ya mwisho na kuwaaga kama
nilivyoingia," aliongeza.
Nguli huyo aliwaasa wasanii wa nchini kuimba muziki
wenye kujenga kama zamani na si kukimbilia kuimba Bongo Flava, kwani muziki huo
ni wa kisasa, huku akimtaja Diamond kuwa ndiyo mwanamuziki anayempenda zaidi
katika muziki wa kizazi kipya.
0 comments