Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, leo
mchana amefanikisha upatikanaji wa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), kwa wachezaji
wawili wa klabu hiyo kutoka nchini Burundi -Amissi Tambwe na Gilbert Kaze.
Wachezaji hao wawili ambao pia ni tegemeo la timu ya
soka ya taifa ya Burundi (Intamba Murugamba), hawakucheza katika mechi ya Ligi
Kuu ya Tanzania iliyochezwa jana kutokana na kutokamlika kwa uhamisho huo,
jambo lililoleta usumbufu mkubwa kwa benchi la ufundi, wachezaji wenyewe,
uongozi na wapenzi na washabiki wa klabu.
Rage aliondoka jijini Dar es Salaam jana usiku na
imechukua chini ya saa 24 kuweka kufanikisha suala hilo. Katika taarifa yake
kwa wana Simba, Mbunge huyo wa Tabora Mjini alisema amelazimika kuingilia kati
suala hilo kwa sababu lilihusu baadhi ya taratibu muhimu za Shirikisho la Soka
Duniani (FIFA) na ukweli kwamba viongozi wa Vitalo, klabu waliyotoka wachezaji
hao hawakuwa mjni na hivyo kuchelewa kwao kungeigharimu Simba.
"Kila walipokuwa wakipigiwa simu kwa takribani
siku tatu mfululizo walikuwa wakisema kwamba wako milimani. Sasa hawa watu wa
Burundi wakikwambia wako miliman wanamaanisha wameenda kijijini kwao. Kuongea
kwa simu pekee kusingetosha na ndiyo Kamati ya Utendaji ya Simba iliomba niende
mwenyewe Burundi ili suala hili liishe," alisema.
Hii ni mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa
kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa
wachezaji wa kimataifa. Miaka miwili iliyopita, Mwenyekiti huyo alilazimika pia
kusafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa
mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo.
Kutokana na kupatikana kwa ITC hizo, Kaze na Tambwe
sasa wataruhusiwa kucheza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIljoro ya
Arusha iliyopangwa kufanyika Jumatano ijayo mjini Arusha. Klabu ya Simba tayari
imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Joeph Owino na
Abel Dhaira, walicheza katika mechi ya jana kutokana na kukamilisha taratibu
zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
0 comments