Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah 'King' Kibaden
BAADA ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers
ya Tabora, timu ya Simba imewasili mkoani Arusha kwa ajili ya mechi yao ya
kesho dhidi ya JKT Oljoro, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
mjini humo.
Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani kwa njia
ya simu jana, Kocha wa Simba, Abdallah 'King' Kibaden, alisema anashukuru
wamefika salama na wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
Kibaden alisema anaamini muda waliotumia kufika
Arusha unatosha kujipanga, ambapo wamewasili mjini humo juzi wakitokea Tabora
moja kwa moja.
"Tutafanya vizuri katika mechi yetu hii licha
ya kuanza vibaya, lakini hiyo ni moja ya matokeo ya mchezo wa soka, tumejiandaa
vizuri na tumeanza kufanya mazoezi mepesi," alisema Kibadeni.
Alisema kupatikana kwa Hati za Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) za wachezaji kutoka Burundi Girbert Kaze na Amiss Tambwe kutasaidia
kukiimarisha kikosi chake.
"Naamini kikosi changu kipo tayari kwa ajili ya
mchezo huu dhidi ya Oljoro na ukizingatia wachezaji wangu wawili wamepata ITC,
hivyo nina kila sababu ya kuibuka na ushindi katika mechi hiyo," aliongeza
Kibadeni.
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, alisema
wameona upungufu uliojitokeza katika mchezo wao uliopita dhidi ya Rhino na
kwamba wameshaufanyia kazi hususani suala la kipa wao, Abel Dhaira la kufungwa
mabao yanayofanana.
Aliwataka mashabiki wa Simba wa jijini humo
kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao na wasikatishwe tamaa na matokeo ya
sare waliyoyapata ugenini na kwamba ugenini kunakuwa na mambo mengi.
0 comments