KLABU ya soka ya Yanga, leo imewasilisha rasmi
pingamizi juu ya adhabu aliyopewa winga wao, Mrisho Ngassa na kusisitiza ni lazima
watani zao wa jadi, Simba waadhibiwe kwa kumsainisha mchezaji huyo akiwa katika
mkataba na Azam FC.
Ngassa amefungiwa kucheza mechi sita na Kamati ya
Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji na kutakiwa kurejesha fedha za usajili
alizopewa na klabu ya Simba Sh. 30 milioni na fidia ya asilimia 50 ya kiasi
hicho alichopewa baada ya kusaini mkataba wakati akitokea Azam kwa mkopo.
Winga huyo aliyeruhusiwa kuichezea Yanga msimu ujao,
alianza kuitumikia adhabu hiyo katika mechi iliyopita ya Ngao ya Jamii dhidi ya
Azam.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako, aliiambia
blog ya Nyumba ya Michezo na Burudani wameshalifanyia kazi suala hilo
na kuamua leo au kesho watawasilisha rasmi pingamizi hilo.
"Tunawasilisha pingamizi kwa kamati ya rufaa
kupinga uamuzi wa kamati ya Mgongolwa (Alex) kumpa Ngassa adhabu hiyo wakati
tulikuwa sahihi kumsajili na tulifuata taratibu zote zinazotakiwa,"
alisema Mwalusako na kuongeza;
"Sisi tulimsajili Ngassa akiwa huru, lakini
wenzetu (Simba) waliingia makubaliano naye akiwa ndani ya mkataba uliobaki
miezi tisa kumalizika, tunashangaa hawajafungiwa."
Alisema kwa kanuni za usajili zinasema klabu inapaswa
kufanya mazungumzo na mchezaji akibakisha miezi sita kabla ya mkataba
kumalizika na ndicho walichofanya wao, sasa wanashangaa kupewa adhabu.
Alipoulizwa kuhusu Ngassa kuchukua fedha Simba na
kusaini kwao, alisema suala hilo ni binafsi na ilipaswa Simba, Yanga na
mchezaji husika kulijadili, lakini lilipelekwa sehemu ambayo si sahihi
kujadiliwa.
Mwalusako alisema kutokana na hilo, ndiyo maana hata
barua waliyoipata kutoka kwa kamati hiyo inayoelezea adhabu ya Ngasa haijawekwa
wazi ni kifungu kipi kimetumika kumuadhibu mchezaji huyo.
Katibu huyo alisema mchezaji huyo ameonewa kwani
kama zingefuatwa kanuni hata Simba ingelazimika kukumbwa na rungu hilo, na
alisisitiza wapo tayari kukaa meza moja na watani zao kujadili suala hilo.
0 comments