Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero akifunga bao la pili.
KOCHA mpya wa klabu ya Manchester City, Manuel
Pellegrini ameanza vizuri kibarua chake baada ya kuitandika Newcastle mabao 4-0
katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya England.
Kwa ushindi huo Manchester City ndiyo inayoshikiria
usukani wa ligi hiyo wakiwa na poindi tatu na mabao manne ya kushinda wakifuatiwa
na Mahasimu wao watoto wa Moyes (David), Manchester United wenye pointi sawa lakini
wao wameruhusu bao moja la kufungwa huku wakishinda manne.
Kikosi cha Pellegrini ambacho kilikuwa katika uwanja
wa nyumbani wa Etihad, kilianza kuwainua mashabiki wake dakika ya sita ya
mchezo huo kwa bao safi lililofungwa na kiungo wake, David Silva akimalizia
pasi nzuri kutoka kwa mshambuliaji mwenye nguvu wa klabu hiyo, Edin Dzeko.
Sergio Aguero akishindilia msumali wa pili kwa
Newcastle dakika ya 22 baada ya kufanya shambulio la ghafla na kumtoka beki wa
timu hiyo na kuachia shuti ambalo lilijaa moja kwa moja wavuni na kumshinda
kipa, Tim Krul na kujaa wavuni.
Newcastle ambao walimaliza mchezo huo wakiwa 10
baada ya Steven Taylor kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Aguero,
walijikuta wakiongezwa bao la tatu dakika ya 50 lililofungwa na Yaya Toure kwa
faulo ya moja kwa moja iliyojaa wavumi kabla ya Samir Nasri kufunga pazia ya
mabao kwa timu yake dakika ya 75.
Man City walionekana kuwa tishio kwa wapinzani wao
dakika zote za mchezo kutokana soka safi waliolionyesha, huku wachezaji wake
wapya waliotua klabuni hapo msimu huu, Fernandinho na Jesus Navas wakitakata
katika eneo la kiungo.
0 comments