Kikosi cha wachezaji wa Yanga
HATIMAYE uongozi wa Yanga umefanikiwa kuwalipa sh.
milioni 50 kati ya milioni 100, wachezaji wake ikiwa ni sehemu ya ahadi yao ya
kutwaa ubingwa msimu uliopita.
Mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu
uliopita, na Yanga kutwaa ubingwa huo, uongozi uliwaahidi sh. milioni 100,
ikiwa ni motisha kwa ajili ya kutwaa ubingwa huo uliokuwa ukitetewa na Simba,
ambao walimaliza wakiwa nafasi ya tatu.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga, ambaye hakutaka
kuandikwa jina lake gazetini, aliiambia Nyumba ya Michezo na Burudani Dar es
Salaam jana kuwa uongozi wao umefanikiwa kuwalipa milioni 50, huku ukiwaahidi
kuwamalizia milioni 50 nyingine ndani ya wiki hii.
"Sisi tulikuwa tunaudai uongozi wetu milioni
100, kwani walituahidi, na wameamua kutulipa nusu, na iliyobaki wamesema
watatumalizia ndani ya wiki hii," alisema mchezaji huyo nyota wa kikosi
hicho.
Aidha nyota huyo alisema, fedha hizo zilikumbushwa
na nahodha wao, Nadr Haroub 'Cannavaro' Jumamosi iliyopita kabla ya kwendwa
uwanjani katika mechi yao na Ashanti, ambapo Yanga ilishinda mabao 5-1.
Mchezaji huyo aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na
kambi makao makuu ya klabu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kesho
dhidi ya Coastal Union utakaipigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo viongozi wa Yanga walishindwa kupatikana
kuthibitisha kama taarifa hizo, lakini simu ya mkononi ya Makamu Mwenyekiti,
Clemence Sanga na Katibu wake, Laurence Mwalusako bado hazina majibu.
0 comments