Na Erasto Stanslaus
SAKATA la usajili wa kiungo mshambuliaji wa timu ya soka ya
taifa, Mrisho Ngassa linaonyesha kwamba kanuni za mikataba na usajili wachezaji
wa mkopo zinatakiwa kuongezewa makali.
Simba iliposoma kanuni
hizo iligundua upenyo hivyo baada ya kumchukua Ngassa kwa mkopo akitokea Azam
FC iliamua kuingia mkataba mpya juu kwa juu.
Yanga nao baada ya
kujua wamewahi kuitibulia Simba kwa usajili wa Kelvin Yondani na Mbuyu Twite
bila kuadhibiwa, ilijitosa kukamilisha usajili wa Ngassa.
Hapo ndipo Kamati ya Sheria
na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TTF) ikanasa. Kwa woga
haikutaka kuiadhibu Yanga kwa faulo iliyofanya, na kwa woga haikutaka kutupilia
mbali mkataba wa Simba.
Kamati hiyo ikaamua kupita
njia salama. Imetambua mkataba wa Ngassa na Simba na imetambua pia mkataba wa
Ngassa na Yanga, lakini kwa vile Msimbazi hawakukamilisha fomu za usajili,
kamati ikamhalalisha kukipiga Jangwani ambako taratibu za usajili
zilikamilishwa.
Hata hivyo, TFF
imemtaka Ngassa kurejesha Sh. 30 milioni alizopewa kama kishika uchumba wa yeye
kuichezea klabu hiyo msimu huu na Sh. 15 milioni kama fidia kwa Simba.
Ameadhibiwa pia kutocheza mechi sita na hatacheza mpaka alipe fedha hizo.
Ngassa hana fedha hizo,
na ilivyo Yanga imejiona imeadhibiwa, sasa inahaha kutaka mchezaji huyo
asiadhibiwe. Yanga hata kama itakata rufani, katika sakata hili, kikanuni
haihusiki.
Kwa kuwa TFF inatambua
usajili wa mchezaji baada ya kukamilisha fomu mama za usajili zenye picha na
saini, Simba inaweza kukataa haikumsajili Ngassa akiwa na usajili wa Azam.
Lakini hatua ya klabu
hiyo kuingia naye mkataba 2 Agosti 2012 ni kosa kikanuni kwani huko ni kufanya
mazungumzo kabla ya muda unaotakiwa.
Kwa mujibu wa Kanuni za
Usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom, Simba ilipaswa kuadhibiwa kwa kosa
la kuingia mkataba juu ya mkataba wa Ngassa na Azam.
Ibara ya 5 ya Kanuni za
Fifa kuhusu Usajili na Hadhi ya Wachezaji sehemu ya 3 inasema kuwa “Mchezaji
anaruhusiwa kuichezea klabu moja tu kwa wakati.”
Kanuni ya 37 kuhusu usajili sehemu ya 2
inasema “Mchezaji anaweza kusajiliwa na klabu moja kwa wakati huo na sio
vinginevyo”.
Kanuni
ya 44 kuhusu Masharti ya mikataba kati ya
wachezaji na klabu
sehemu ya 2 inasema klabu
inayotarajia kuingia mkataba na mchezaji wa kulipwa haina budi kuiarifu klabu
yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo wa
kulipwa. Mchezaji wa kulipwa atakuwa huru tu kuingia mkataba na kilabu nyingine
iwapo mkataba wake na kilabu yake ya sasa umekwisha au utakwisha baada ya miezi
sita (6). Uvunjaji wowote wa sharti hili utastahili vikwazo vinavyofaa.
Makubaliano
yaliyokuwepo kati ya Simba na Azam yalikuwa ya Ngassa kucheza kwa mkopo lakini
kwa ujanjaujanja wakaingia mkataba usiohusika.
Vilevile, Ibara ya 42
ya Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom kuhusu Kuazimwa kwa mkopo kwa wachezaji wa
kulipwa zinaeleza wazi.
(1) Mchezaji wa kulipwa anaweza kuazimwa kwa
mkopo na klabu nyingine kwa msingi wa makubaliano ya maandishi kati yake na klabu
zinazohusika. Uazimwaji huo wa mkopo utafuata sheria zilezile zinazotumika
katika uhamisho wa wachezaji, yakiwemo masharti ya fidia ya mafunzo na utaratibu wa mshikamano.
(2)
Kufuatana na Ibara ya 5(3), ya kanuni
za FIFA kipindi cha chini cha mchezaji kuazimwa kwa mkopo kitakuwa ni muda kati
ya vipindi viwili vya usajili.
(3) Klabu itakayompokea mchezaji kwa msingi wa kuazimwa
kwa mkopo haina haki ya kumhamishia katika klabu nyingine bila ya idhini ya
maandishi ya klabu iliyomwachia mchezaji
kwa mkopo na ya mchezaji anayehusika.
Kanuni hizo zote
zinaelezea kwa uwazi masharti ya usajili, lakini si mikataba. Kama mkataba wa
Simba na Ngassa uliochapwa magazetini ni sahihi, Simba ikijua hakuna kifungu
kinachowabana kuhusu mikataba ilimlazimisha Ngassa kutia saini mkataba wa
nyongeza huku akiwa mchezaji halali wa Azam.
Kwa kuwa Simba na Yanga
zimeona matundu katika kanuni za mikataba na usajili, TFF iangalie uwezekano wa
kuboresha kanuni kuzibana klabu hizo zisiendelee kuumiza wachezaji.
Makala
hii imetolewa kwenye gazeti la Mawio
0 comments