KIKOSI cha Simba leo imeonja uchungu wa kufungwa
baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Azam FC mchezo uliochezwa leo
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ambayo huu ndiyo mchezo wao wa kwanza kupoteza
tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado ipo katika nafasi ya tatu ikiwa
na pointi 20.
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la
kuongoza kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Ramadhani Singano ‘Messi’ dakika
ya 13 akimalizia kazi safi ya Zahor Pazi aliyeitoka ngome ya Azam na kupiga
krosi fupi iliyomkuta mfungaji.
Azam waliendelea kulisakama lango la Simba na
kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa Kipre Tchetche dakika ya 45
akimalizia krosi safi ya Erasto Nyoni na kufanya timu zote kwenye mapumziko
zikiwa zimetoshana nguvu kwa bao 1-1.
Kipindi cha pili mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa
lakini Kipre aliizamisha jahazi la Simba baada ya kufunga bao la pili dakika ya
73 baada ya kufanya kazi kubwa ya kupangua ngome ya Simba na kumhadaa kipa,
Abel Dhaira na mpira kujaa wavuni.
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni mara baada ya
mchezo huo alisema amekubali matokeo hayo na kilisababisha ni kutokuwa na
wachezaji wake nyota lakini makosa yaliyofanywa na wachezaji wake ndiyo
yaliyosbabisha kupoteza mchezo huo.
Simba: Abel Dhaira, William Lucian, Issa Rashid,
Hassan Khatib, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla,
Betrum Mombeki, Zahor Pazi/ Sino Augustino na Amri Kiemba/ Edward Christopha.
Azam FC: Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Wazir Salum,
Aggrey Morris. Said Morad/ David Mwantika, Boluo Kipre, Salum Aboubakary,
Humphrey Mieno/ Khamis Mcha, John Bocco, Kipre Tchetche na Joseph Kimwaga.
0 comments