MAKAMU wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja kwa waamuzi
waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar
es Salaam.
Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo
akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza waamuzi hao kwa
kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
“Waamuzi wanapofanya vibaya tunawaadhibu, hivyo
wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia. Vilevile kuwapongeza ni
kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,” alisema Nassib.
Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo hilo ambapo
mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati namba mbili alikuwa
Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden Mbaga.
Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na wanatoka Dar es Salaam ukiondoa Chacha
ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.
0 comments