KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
amekiri kuwa kikosi chake ni kibovu lakini kwa ubovu huo huo waliokuwa nao,
mahasimu wao Yanga watapokea kipigo katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu
Tanzania Bara si chini ya mabao matatu.
Simba ambayo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 15
baada ya kucheza michezo saba, inatarajia kuivaa Yanga katika mchezo wa raundi
ya kwanza utakaochezwa Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Nyumba ya Michezo na Burudani, Julio
alisema kuwa watu wanasema kuwa Simba ni mbivu, wao wanakubali maneno hayo
lakini timu hiyo inayoitwa mbovu ndiyo inayoongoza ligi na katika mchezo wao na
Yanga wataibuka na ushindi mnono si chini ya mabao matatu.
Julio alisema hana wasiwasi na kikosi chake katika
michezo inayoendelea ya ligi hiyo na anaamini kuwa katika mchezo wao na Yanga
wataibuka na ushindi na kuendelea kukaa kileleni mwa ligi hiyo.
Kocha huyo aliyejaliwa kuwa na maneno mengi alisema
kuwa katika kikosi chao hawana matatizo yoyote na wachezaji wao na taarifa
zinzaotolewa zina malengo ya kuibua migogoro isiyokuwa na sababu.
“Simba haina ugomvi wowote kati ya wachezaji na
makocha. Kinachoandikwa ni uzushi mtupu na kuthibitisha hilo tutaendeleza wimbi
la ushindi na kutwaa ubingwa na timu hii ambayo kila mtu anaiona mbovu,”
alisema Julio.
0 comments