RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa kupata Kamati mpya
ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27 mwaka huu kama ilivyopangwa.
“Wazungu wanasema ije mvua au jua, uchaguzi
utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa uchaguzi huru na
wa haki,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye
ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).
Amesema mchakato unakwenda vizuri kilichobaki ni
revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele ya Kamati ya Rufani ya
Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo si kuzuia
watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa za wagombea
yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha inatendeka hata kama ni
kwa mtu mmoja.
Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji 58 ambapo
watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga kuondolewa na
Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao yamepelekwa Kamati ya
Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision) ili kupata mwongozo wa
utekelezaji.
Mwongozo huo umeombwa na Sekretarieti ya TFF kwa
Kamati ya Rufani ya Maadili kwa vile Kamati ya Maadili iliwaona waombaji wanane
wa uongozi waliofikishwa mbele yake kwa makosa ya kimaadili kutokuwa na hatia,
lakini wakati huo huo ikitambua kuondolewa kwao kwenye kinyang’anyiro cha
uchaguzi kulikofanywa na Kamati ya Uchaguzi.
MRADI WA FOOTBALL FOR HOPE KUFUNGULIWA OKTOBA 13
Mradi wa Football for Hope kusaidia watoto na
wasiojiweza kupitia mpira wa miguu uliofadhiliwa na Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) mkoani Iringa utafunguliwa rasmi Oktoba 13 mwaka huu.
FIFA hutoa mradi huo kwa baadhi ya nchi kwa
kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo utawala bora, lakini kwa kupitia taasisi
zisizo za kiserikali (NGOs) ambapo kwa Tanzania umepatikana kupitia taasisi ya
Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care (IDYDCC).
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameishukuru FIFA kwa
msaada huo, kwani ni mkubwa na kuongeza kuwa ni matumaini yake utatumika kwa
lengo lililopangwa.
Amesema mradi huo wa FIFA ambao ni wa kusaidia
watoto kielimu na wasiojiweza kwa kupitia mpira wa miguu haukupita moja kwa
moja TFF ni mzuri kwani moja ya mambo uliofanikisha ni kuwepo jengo na sehemu
ya watoto kucheza.
Ni wastani wa nchi kumi tu duniani kwa mwaka
zinapata mradi huo kutoka FIFA, jambo ambalo Rais Tenga amesema linachangiwa
pia na uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na shirikisho hilo.
KAMATI YA WANAWAKE, TWFA YAPONGEZWA
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA) wamepongezwa kwa kuhakikisha akina mama wanacheza mashindano
mbalimbali.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TFF, Leodegar
Tenga ambapo amesema timu za wanawake zimekuwa zikishiriki katika mashindano
mbalimbali licha ya ukweli kuwa hadi sasa hakuna udhamini kwenye mchezo huo.
Amesema mpira wa miguu unaendeshwa na udhamini na
kuchangia, jambo ambalo linafanikishwa kwa kiasi kikubwa na uwazi katika
matumizi ya fedha, jambo ambalo hivi sasa lipo ndani ya TFF.
Rais Tenga amesema baada ya kuanzisha Kamati ya
Ligi, hivi sasa TFF inapata asilimia 4.5 tu ya mapato ya mechi za ligi kutoka
asilimia 33 iliyokuwa ikipata wakati anaingia madarakani mwaka 2004.
Amesema asilimia hiyo 4.5 haiwezi kuendesha mpira na
ndiyo maana nguvu zinaelekezwa katika kutafuta wadhamini na kuchangia. Pia TFF
inatoa zaidi ya asilimia 15 ya Fedha za Msaada wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
(FAP) kutoka FIFA kwenye mpira wa miguu wa wanawake ambapo ni nchi chache
zinazofikia kiwango hicho.
Hivyo, ametoa mwito kwa kampuni kujitokeza kudhamini
au kuchangia timu za Taifa za mpira wa miguu za wanawake ambazo zinashiriki
mashindano mbalimbali mwaka huu, kwani gharama za kuziendesha ni kubwa.
Timu ya wakubwa (Twiga Stars) inacheza mashindano ya
mchujo ya Fainali za Afrika (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia wakati
ile ya chini ya miaka 20 inacheza mashindano ya Dunia ambayo fainali pia
zitachezwa mwakani nchini Canada.
0 comments