TIMU ya Yanga imeendeleza wimbi la ushindi wa mabao
matatu baada ya leo kuitandika Mgambo Shooting mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi
Kuu Tanzania bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Yanga kushinda
mabao matatu dhidi ya Rhino Rangers na leo Mgambo, huku ikishinda tatu dhidi ya
Simba lakini wakafanikiwa kusawazisha.
Yanga ambao walikuwa uwanjani bila ya nyota wake, Haruna
Niyonzima, walipata bao la kwanz kupitia kwa beki wake kiraka, Mbuyu Twite
dakika ya 32 kwa shuti kali ya faulo kufanya timu yake kwenda mapumziko wakiwa
mbele.
Dakika 52 Yanga waliongeza bao la pili kwa mkwaju wa
penalti kupitia kwa Hamis Kiiza na kufunga bao lake na nane na kuwa sawa na
kinara wa mabao Amisi Tambwe wa Simba, baada ya beki wa kipa wa Mgambo, Godson
Mmasa kumwangusha mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu.
Kavumbagu alishindilia msumali wa tatu kwa Mgambo
kwa shuti kali lililomshinda kipa Mmasa na kutinga wavuni na kufanya Yanga
kupata ushindi huo wa mabao matatu kwa mechi mbili mfululizo.
Kwa matokeo hayo Yanga wamepanda hadi nafasi ya tatu
na kuiacha Simba nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 22 wakiwa nyuma ya
Mbeya City na Azam ambao wote wanapointi 23 huku wakitofautiana mabao ya
kufunga na kufungwa.
Mbeya City nao wameitandika ndugu zao wa Prisons kwa
mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya Peter Mapunda dakika ya 67 na Deogratius
Julius dakika ya 79.
Katika mchezo mwingine leo Rhino Rangers waliutumia
vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu,
mfungaji akiwa Abbas Mohamed dakika ya 71.
0 comments