LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi
tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.
Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa
ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons
inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo
wa ligi hiyo.
Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye
msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo
katika mechi yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo
Shooting inalazimika kuifunga Simba.
Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita
dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya
Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo
kwa wapinzani wao Tanzania Prisons.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh.
8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari
maalumu kuanzia saa 4 kamili asubuhi.
Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba
kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na
Mganda Jackson Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage.
Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya
pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa
mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya
nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.
Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa
Yanga kuibuka na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi
dhidi ya Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha
timu 14.
Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha
mechi kati ya Ashanti United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa
Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers
(Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na
JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu,
Turiani).
Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam
TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa
Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu
itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.
FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu
inaendelea wikiendi hii ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli
na Mlale JKT itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa
Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja
wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A
zitakazochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu).
Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa
(Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa
kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad.
Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho
(Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma
utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.
Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja
wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini
Musoma utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.
0 comments